Siasa

Polisi wazima mkutano wa Mudavadi mjini Mbale

October 3rd, 2020 1 min read

NA DERRICK LUVEGA

KINARA wa chama cha Amani National Congress (ANC) Bw Musalia Mudavadi alilazimika kuhutubia wafuasi wake kando ya barabara mjini Mbale, Kaunti ya Vihiga baada ya polisi kufunga uwanja wa Idavaga ambapo mkutano wa kisiasa wa vijana ulikuwa ufanyike Jumamosi.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alikuwa amepanga kuzindua tovuti ya Vuguvugu la Vijana wa Mulembe kwenye mkutano huo uliokuwa uhudhuriwe na Bw Mudavadi lakini polisi waliwazuia kuingia kwa uwanja huo.

Barabara zote zinazoelekea uwanjani humo zilifungwa, huku magari yakielekezwa kutumia barabara kuu ya kutoka Kakamega kwenda Kisumu.

Maafisa hao wa polisi walisema Bw Malala hakuwa na cheti cha mkutano huo, lakini akadai polisi wanatumika kusambaratisha juhudi zake za kuunganisha vijana wa eneo hilo.

Bw Malala alitaja kuwa mkutano huo ulizimwa na wanasiasa ambao hawafurahishwi na uamuzi wake wa kuungana tena na Bw Mudavadi.

“Mkutano huu umesimamishwa kutokana na msimamo wangu dhabiti kuhusu ugavi wa pesa za kaunti,” alisema.

 

TAFSIRI NA FAUSTINE NGILA