Habari Mseto

Polisi zaidi watumwa kulinda Wakenya Krismasi

December 25th, 2020 1 min read

Na Winnie Atieno

SERIKALI imewatuma maafisa zaidi wa usalama kushika doria makanisani, mahoteli na katika fuo eneo la Pwani wakati wa sherehe za Krismasi.

Kulingana na Mshirikishi wa Serikali Kuu eneo la Pwani, Bw John Elungata na kamanda wa polisi anayesimamia eneo hilo Bw Gabriel Musau, askari jela 500 wametumwa kusaidiana na maafisa wa polisi katika kudumisha usalama.

“Tumeimarisha usalama sehemu ambapo wageni wengi hufurika ikiwemo bustani ya Mama Ngina, kisiwani Chale, Watamu na Shela ili kuhakikisha utulivu na amani. Wageni wanaozuru Mombasa, Lamu, Tana River, Taita Taveta, Kwale na Kilifi wasiwe na wasiwasi kwani usalama umedumishwa. Lakini lazima kila mtu azingatie masharti ya kuzuia corona,” akasema Bw Elungata.

“Tumeshirikiana na NTSA ili kuhakikisha magari yote ya umma na yale ya kibinafsi yanafuata kanuni za trafiki. Msiendeshe magari kwa kasi. Ajali nyingi hutokea wakati dereva ni mlevi, anaendesha gari kwa kasi, gari ni bovu au limejaa,” akasema Bw Musau.

Aliwatahadharisha wale watakaovunja sheria kwamba watatiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani.“Hatutaki kuona mtu yoyote au gari ifikapo saa nne usiku. Baa na sehemu zote za burudani zifungwe ifikapo saa tatu usiku. Sheria za kafyu lazima zifuatwe,” akaongeza.