Polo 2 wakabana demu akijifungua

Polo 2 wakabana demu akijifungua

Na TOBBIE WEKESA

KABARNET, BARINGO

POLO alipigwa na butwaa alipowasili katika hospitali moja hapa na kumpata jamaa mmoja akimsubiri mkewe kujifungua.

Inadaiwa jamaa huyo alifika hosipitalini baada ya kujuzwa na mwanadada kuhusu kulazwa kwake hospitalini baada ya kupelekwa na mumewe kujifungua.

Kulingana na mdokezi, jamaa alikuwa mpango wa kando wa kidosho.

Inadaiwa kwamba mimba aliyokuwa amebeba kipusa haikuwa ya mumewe bali ya mpango wa kando.

“Niko hospitalini karibu najifungua. Njoo umuone mwanao kabla ya mume wangu kufika,” mwanadada alimweleza jamaa kwa simu.

Duru zinaarifu kwamba jamaa aliwasili asubuhi na mapema hospitalini.

Aliarifiwa na wahudumu atulie katika chumba cha mapokezi amsubiri demu.Inasemekana haikupita muda mrefu kabla ya mume wa mwanadada kufika.

“Nimemletea mke wangu chakula. Nilimleta huku jana jioni kujifungua,” polo alimueleza mlinzi aliyekuwa kwenye lango.

Mlinzi alichanganyikiwa kiasi.

“Kuna mtu aliingia hapa dakika chache zilizopita. Aliandikisha hapa kuwa anaenda kumuona huyo huyo mwanamke unayedai kuwa mkeo,” mlinzi alimueleza polo.

Inadaiwa polo alianza kuingiwa na wasiwasi.

“Jina lake ndilo hili hapa. Sura yake naijua vizuri sana. Njoo twende tumtafute,” mlinzi alimueleza polo.

Walipofika katika chumba cha mapokezi, walimpata polo ametulia.

“Bosi ulisema unakuja kumuona nani?” mlinzi alimuuliza jamaa.

Inasemekana jamaa alisimama na kuanza kufoka.

“Nimekuja kumuona mrembo wangu. Alinipigia simu akidai aliletwa hapa kujifungua,” jamaa alifoka.

Inasemekana mlinzi alimlazimisha jamaa aondoke chumbani ili wasuluhishe mambo nje ya hospitali.

“Hiyo mimba aliyobeba ni yangu. Sitaki kumuona huyu mtu hapa,” jamaa alifoka.

Habari zilizotufikia zinasema makalameni walirukiana na kuanza kurambishana changarawe.

Ilimlazimu mlinzi kuingilia kati.

You can share this post!

AKILIMALI: Hivi viazi vitamu ni spesheli kwa njia moja...

Siraj apigania kupata namba Harambee Stars