Dondoo

Polo aacha kazi eti bosi anamnyemelea

February 10th, 2018 1 min read

KABATI, MURANG’A

Na TOBBIE WEKESA

KALAMENI mmoja aliyekuwa akifanya kazi ya shambani katika boma la eneo hili, aliwashangaza wengi alipoacha kazi akidai mke wa mdosi alikuwa akimnyemelea.

Kulingana na polo, mama alipenda sana kumpa “mshene” kumhusu bwana yake. Jamaa alidai mke wa bosi alipenda kumpigia polo simu akisema alitaka kumpa salamu tu.

Duru zinasema mara kwa mara, mdosi alipokosa kurejea nyumbani kwake, mkewe alikuwa akimpigia polo simu na kumuelezea jinsi alivyokuwa akipigwa na kibaridi usiku.

Alifichua kwamba mwanamke huyo alikuwa akimtisha akubali mambo yake au amfute kazi. Polo aliamua kumpuuzilia mbali kipusa japo wasiwasi wake ulikuwa huenda mdosi akagundua mkewe humpigia simu wakati wa usiku.

Kulingana na polo, mdosi hangeamini kuwa ni mkewe aliyekuwa akimsumbua. Penyenye zinasema mdosi alijulikana kijiji kizima kama mtu asiyependa mzaha na yeyote aliyechezea mali yake.

Kwa kuhofia kupewa adabu kali, polo aliamua kufunganya virago na kwenda zake.

“Huyu mwanamke atanisababishia balaa. Bwana yake akisikia haya mambo, hatanielewa. Heri nichukue tahadhari ya mapema,” polo alisema akianza safari.
Wenyeji wa hapa walishangaa kumuona mtu aliyefanya kazi kwa unyenyekevu kwa muda mrefu akiondoka ghafla.

“Mimi ninataka kuishi kesho. Huyu mwanamke ameninyemelea kwa muda mrefu sana na mimi sitaki maneno yake,” polo aliwaeleza majirani. Vilevile aliwaeleza majirani jinsi mwanamke huyo alivyokuwa akimpigia simu usiku akimuomba ampe joto.

Polo alidai kwamba licha ya kukataa wito wa mama, mdosi hangeshawishika na maelezo yake iwapo angegundua kilichokuwa kikiendelea.
“Acha amnyemelee mtu mwingine lakini mimi sitaki majeraha,” polo aliwaaga majirani na kuenda kabisa.