Dondoo

Polo ahama baada ya kufumania mke akitafunwa na rafiki

July 3rd, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

USENGE, BONDO

Kalameni mmoja wa eneo hili aliwashangaza wengi alipoamua kugura boma baada ya kumpata mkewe akila uroda na rafiki yake. Inasemekana polo alifunganya virago na kuondoka bila kumueleza yeyote alikokuwa akienda.

Kulingana na mdokezi, polo alikuwa ameondoka nyumbani kuhudhuria mkutano uliokuwa umeandaliwa na wazee wa ukoo wake.

Duru zinaarifu kwamba mkewe naye alitumia fursa hiyo kumualika jamaa ambaye wengi walikuwa wakimfahamu kama rafiki wa karibu wa polo.

Inadaiwa mwanadada na jamaa huyo waliingia kitandani na kuanza kulishana tunda bila wasiwasi wowote. Penyenye zinasema kabla ya muda mfupi, polo aliwasili bila kubisha.

Mdokezi anasema kwamba polo alimkuta jamaa aliyemchukua kama mwandani wake akichovya asali yake bila wasiwasi.

“Mnafanya nini,” polo alifoka naye jamaa akamkodolea macho tu asijue la kufanya. “Unawezaje kufanya tendo kama hili kwenye kitanda changu,” polo alizidi kumfokea mkewe.

Inasemekana polo aliwaeleza waendelee na shughuli zao. “Nimekuchukua kama rafiki wangu wa karibu sana. Sikujua unanikula kichinichini. Nimekuachia mke huyo ukitaka kumuoa mchukue,” polo alimfokea jamaa.

Penyenye zinasema polo alianza kukusanya vitu vyake huku jamaa akipata mwanya wa kuhepa. “Mwambie mpango wako wa kando arudi akuoe.

“Hata nyumba na kitanda nimemuachia. Mimi naenda zangu,” polo alimueleza kipusa huku akianza safari. Kulingana na mdokezi polo alimueleza kila aliyekutana naye sababu ya kugura boma lake. Wenyeji walishangazwa sana na tukio hilo.

“Huyu mwanamke amenikosea heshima sana. Siwezi kuishi naye tena katika chumba kimoja,” polo aliwaeleza majirani.

Inasemekana mkewe alifunganya virago na kutoweka boma likabaki bila mtu.