Dondoo

Polo ajuta kujifanya dume la kupokonya wenzake mademu

February 24th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KARIOBANGI, NAIROBI.

Polo mmoja alikemewa vikali na wenyeji wa hapa kwa kujifanya jogoo wa jijini na kuwapokonya wapenzi wao.

Inasemekana kwamba licha ya polo kuwa mgeni eneo hili, alionyesha waziwazi alivyokuwa mkali wa kuchota warembo.

Inadaiwa baada ya kuwasili kwa mjomba wake aliyekuwa akiishi hapa, jamaa alianza kutumia fimbo yake ipasavyo kuwanyorosha warembo kwenye ploti na hata ploti jirani.

Inasemekana jamaa alikuwa akijisifu jinsi alivyokuwa mkali kwa kuwachota vidosho na kuwapandisha mizuka. Kila mtu alishangazwa na namna alivyokuwa akiwashughulikia vipusa kwani weledi wake ulionekana wazi.

“Huyu jamaa ametoka mashambani juzi. Amekuja na makeke sana,” kalameni mmoja alidai. Penyenye zinasema makalameni kwenye ploti alikoishi polo na ploti nyingine jirani hawakufurahishwa na tabia yake.

Inasemekana mambo yalimwendea kombo alipojaribu kumrushia ndoano mrembo fulani ambaye mchumbake alikuwa akiishi kwenye ploti jirani.

Inadaiwa makalameni walipopata habari kwamba wao wamo hatarini kupokonywa wachumba, walimvamia polo na kutisha kumpa kichapo.

“Boss, unatuona sisi ni bongo lala? Ama unafikiri sisi ni wajinga,” kalameni mmoja alimkaripia polo. ? Polo alibakia kuwa zuzu asijue la kufanya. “Achana na wasichana wetu. Kama ulikuwa bingwa katika sekta hiyo kule kijijini, jua hili ni jiji. Kuja polepole,” polo alizomewa.

Habari zilizotufikia zinasema polo naye alianza kuwafokea makalameni. “Kama nyinyi mmelala mnataka nifanye nini? Warembo wenyewe wananitaka,” polo alisema.

“Una ujinga sana. Tangu lini jogoo wa vijijini akawika jijini? Hapa si kwenu,” makalameni walisema huku wakitisha kumuadhibu polo.

Polo aliwaomba msamaha lakini hakusikizwa. “Huwezi kuja hapa tu juzi na kuanza kuonyesha ubingwa wako kitandani tukiangalia,” makalameni walimuonya polo.