Dondoo

Polo ajuta kutomasa mama pima kazini

July 24th, 2018 1 min read

NA TOBBIE WEKESA

Mukuru, Nairobi

Kizaazaa kilizuka eneo hili baada ya makalameni kumkabili polo walipomkuta akitaka kumbusu mama pima.

Inasemekana makalameni hao walikasirika sana walipogundua kwamba jamaa ndiye aliyefanya wasihudumiwe upesi kwa kumpapasa mama pima.

Kulingana na mdokezi, makalameni hao walifika kwa mama pima asubuhi na mapema ili kupata dozi. Kilichowashangaza ni jinsi mama pima alivyojikokota kuwahudumia. “Kwani leo huyu mama hataki hela zetu?” kalameni mmoja alisikika akisema.

Makalameni waliamua kumpa mama pima muda kidogo. “Ama ameshakuwa tajiri? Acha tumpe muda pengine anajitayarisha kuamka,” makalameni walisema.

Duru zinasema baada ya kungoja kwa muda mrefu, makalameni waliamua kuchungulia ndani ya nyumba ya mama huyo ili kubaini kilichokuwa kikiendelea.

Penyenye zinasema walimuona polo kwenye kochi bila wasiwasi wowote. Kando yake mama pima alikuwa ameinamisha kichwa chake kwenye bega la jamaa.

“Angalia huyu jamaa. Tunaendelea kupigwa na baridi tukingoja pombe kumbe yuko hapa kumzubaisha mama yetu,” kalameni mmoja alisikika akisema.

Makalameni walianza kumfokea jamaa. “Bosi, hatuwezi kuumia kwa sababu yako. Toka hapa haraka,” makalameni walichemka.

Kutokana na aibu, mama pima aliwahimiza makalameni watulie ili awape kinywaji. “Kazi yake tunaijua. Yeye na wanawake hawaachani. Atoke haraka ama tumpe adabu,” mapolo walifoka.

Habari zilizotufikia zinasema makalameni walianza kutafuta viboko tayari kumuadhibu jamaa. “Kama anataka mtu wa kupapasa aje jioni. Hawezi kutupotezea wakati hapa. Hata sisi tuna shughuli nyingine za kufanya,” makalameni waliteta.

Inadaiwa jamaa alipoona mapolo wakiingia kila mmoja akiwa na kiboko, aliamua kuchana mbuga kuhepa aibu.