Dondoo

Polo ajutia kupeleka mkewe kwa mganga

July 23rd, 2018 1 min read

Na SAMMY WAWERU

SERGOIT, ELDORET

Jombi mmoja wa kijiji hiki, alijuta kwenda kwa mganga kutafuta ndumba atulize hasira za mkewe, mwanadada alipochotwa na “daktari ” huyo.

Yasemekana mganga alitumia fursa hiyo kumnyemelea mke wa jamaa wakawa wapenzi.

Kulingana na mdokezi, mke wa jamaa ni mkali na huwa hampi jombi nafasi ya kuongea, hasa anapokosea.

“Mzee akifika kwake akiwa amechelewa, boma huwa halikaliki,” alisema mdokezi.

Jamaa alipoona mkewe amemkalia kupita kiasi, aliomba ushauri kutoka kwa wazee wenza waliomuelekeza kwa mganga.

“Nina mganga mmoja maarufu atakayetuliza mkeo,” mzee mmoja alimweleza.

Yasemekana kalameni hakupoteza muda, alimwaga mtama kwa mganga yule. “Huyu mke wangu ameninyima amani kabisa, hata tunda la ndoa ninapata mara moja kwa mwezi au hata ninanyimwa kabisa,” polo alimsimulia mganga.

Yasemekana mganga alimhakikishia kuwa angezima ghadhabu za mkewe iwapo angemshawishi wafike kwake pamoja. Kulingana na mdokezi kalameni alifanya juu chini, akamhadaa mkewe kuwa alihitaji kumpeleka ziara.

Mama huyo alijawa na furaha, wakapanga siku maalumu wakaenda zao. “Sasa ninaona umetambua mimi ndiye mkeo,” alisema mama huyo kwa tabasamu.

Ziara iliishia bomani kwa mganga aliyewafanyia matambiko. Wanandoa wale waliondoka kwa mganga mke akilalamika kuwa hiyo haikuwa ziara aliyotarajia.

Duru zinasema mama huyo kwa sasa amekuwa mgeni wa karibu kila siku kwa mganga, na kwamba uhusiano wa mapenzi tayari umeota.

Inasemekana akitoka kazini, jambo la kwanza analofanya ni kupitia kwa mganga hadi saa tano za usiku.

Minong’ono imeenea kijijini humo kuwa wawili hao ni wapenzi, na tayari imefikia polo. Baadhi ya watu wanasema huenda mganga alitumia ndumba zake kumchota mama huyo ambaye ni mwalimu.