Polo akarabatia jirani kitanda kisilie

Polo akarabatia jirani kitanda kisilie

Na MWANDISHI WETU

Kangemi, Nairobi 

Jombi mtaani hapa ambaye ni seremala tajika aliamua kukarabati kitanda cha jirani yake bila malipo ili kiache kumkosesha usingizi. Jamaa alimwambia jirani hakuwa akipata usingizi kutokana na kelele za kitanda chake.

“Jirani, mimi unijuavyo ni seremala. Niko tayari kukarabati kitanda chako hadi kiwe imara. Usiwe na wasiwasi malipo utayatoa wapi kwani nimeamua kukifanyia kazi bila kudai shilingi hata moja kutoka kwako,” seremala alimshangaza jombi.

Seremala huyo alikuwa ameumia siku nyingi. Hakuwa akilala na alipojaaliwa kulala labda kwa dakika chache. Jirani, kijana mwenye umri wa miaka ishirini na saba na ambaye hakuwa ameoa, alimtaabisha sana. Kila siku nyumbani humo alileta mwanamke na usiku kucha ikawa ni ngoma zisizo na mwisho. Ajabu ni kwamba kitanda hicho kilichopokea wageni sampuli sampuli, hakikuwa kitanda thabiti. Kilikuwa legevu.

Kila jirani alipoingia uwanjani kucheza, seremala aliamshwa na sauti za kitanda kutishia kuvunjika zikizidi zile za wachezaji. Kitanda hicho kiliteta kwa saa nyingi na kila siku gemu ilipopigiwa firimbi kuanza, seremala akawa akisubiri kusikia kikivunjika na kuwatupa wote sakafuni.

Zilipita siku nyingi, seremala akikosa usingizi hadi ile siku aliamua kuchukua hatua.

“Jirani, naomba niondoke na kitanda chako nitakurejeshea jioni. Najua kimelegea nami nataka kukiongeza mbao mbili tatu kiwe thabiti,” seremala aliomba. Inasemekana jombi alikubali ombi la seremala na akapeleka kitanda katika karakana yake.

Siku hiyo iliyokuwa sikukuu ya kitaifa, fundi aliitumia vilivyo. Alikikarabati kitanda chote kikasimama imara. Jamaa alienda kukichukua jioni akapata kimefanyiwa kazi.

“Hiki kikiwabeba hata wachezaji kumi, hakitateta tena. Afadhali hivyo nami nipate kulala kama wengine,” seremala alisema.

You can share this post!

Kesi ya kukwepa ushuru wa mfinyo dhidi ya bwanyenye...

Msanii wa nyimbo za injili Mary Njuguna anayewahimiza watu...

F M