Dondoo

Polo akiona kuzuia mkewe kuabudu

November 2nd, 2019 1 min read

Na LEAH MAKENA

TAYARI, MOLO

JAMAA wa hapa alifokewa vikali na mama mkwe kwa kumkataza bibi yake kuhudhuria ibada katika kanisa aliyokuwa akishiriki kabla yao kufunga pingu za maisha.

Kabla ya kufanya harusi, jamaa aliahidi kidosho kuwa angejiunga na kanisa lake lakini akabadilisha nia baada ya mwanadada kuingia boksi.

“Tangu lini ukaona mwanamume akijiunga na kanisa la mkewe? Hata nilikuhurumia sana kukubali kufanyia harusi katika kanisa hilo. Kwa sasa tusisumbuane, kama huwezi kuandamana nami katika kanisa langu, tulia kwa nyumba,” jamaa alimweleza mwanadada.

Kwa zaidi ya mwezi mmoja, kidosho alibaki nyumbani, jambo lililomtia wasiwasi mama yake mzazi na akaamua kumtembelea ili kujua sababu yake kukosa ibada.

Hapo ndipo kidosho alipasua mbarika na kueleza mama jinsi mumewe alivyokuwa akimmzima kila alipotaka kufika kanisani. Mama alipandwa na mori na kuapa kumkabili jamaa kwa kumnyima binti yake uhuru wa kuabudu.

Jioni ya tukio, jamaa alifika na hata kabla ya kuketi mama alianza kumkemea.

“Mbona unatesa binti yangu na ulidai utajiunga na kanisa lake baada ya kuoana? Kama hutaki kuandamana naye si basi umruhusu awe akijipeleka pekee yake?” mama aliteta.

Jamaa alijidhibiti licha ya kupandwa na mori kwani aliogopa kuadhibiwa na watu kwa kujibu mama mkwe vibaya.

Hata baada ya kukemewa, alishikilia msimamo wake na kuapa kutobadilika. Duru zasema kuwa mama alitishia kumchukua binti yake akisisitiza alikuwa na haki ya kuhudhuria ibada bila vikwazo.

Kwa upande wake, kidosho alisalia njia panda asijue la kufanya kati ya kutii mumewe na mama yake.