Dondoo

Polo akodolea macho laana kwa kuchochewa na mke ‘kuchinja’ ng’ombe wa pekee wa mama

February 5th, 2024 1 min read

SAMBURU, KWALE

Na JANET KAVUNGA

JOMBI wa hapa anakodolea macho laana baada ya kumuua ng’ombe wa pekee wa mama yake kwa kumkatakata vipande baada ya kuchochewa na mkewe.

Duru zasema mke wa jamaa hakuwa akipikika chungu kimoja na mavyaa ambaye ni mjane. Juzi, mwanadada huyo alimpigia simu mumewe na kumdanganya kuwa mama yake alikuwa ameachilia ng’ombe wake shambani kuharibu mimea yake.

Bila kuchunguza kujua ukweli, jombi alifika akibeba upanga wenye makali na kumkatakata ng’ombe huyo hadi akamuua.

Kisha alimkabili mama yake na kumtishia vikali akimtaka akome kusumbua familia yake. Inasemekana mama alimkazia macho bila kutamka lolote kisha akatokwa machozi huku jombi akiropokwa. Familia na majirani walimuonya kuwa alikuwa akialika laana kwa vitendo vyake.

***

Kidosho ahepa saluni akiogopa mke wa ‘mpango’

BOMBOLULU, MOMBASA

Na JANET KAVUNGA

KIOJA kilitokea hapa demu alipotoroka mbio mke wa mpango wake wa kando alipofika katika saluni anakofanya kazi.

Demu amekuwa akitoka na mume wa mwanadada huyo kwa muda. Mke wa jamaa hakuwa na habari kuhusu michepuko ya mumewe na siku ya kioja, alifika katika saluni ambayo demu alikuwa akifanya kazi kuhudumiwa.

Akidhani mwanadada alikuwa amegundua uhusiano wake haramu na mumewe, demu alitoka nje haraka na kuhepa.

Wenzake kazini waling’amua sababu yake ya kutoroka na wakamhudumia mwanadada ambaye aliwashukuru kwa kazi bomba na akaenda zake ndipo demu akapigiwa simu na wenzake akarudi kazini na kupumua alipoarifiwa kwamba mke wa jamaa hakuwa akimwandama.