Dondoo

Polo ala kipigo kwa kutongoza wake za watu

June 2nd, 2019 1 min read

NA MIRRIAM MUTUNGA

MITUNGUU, MERU

JAMAA mmoja kutoka eneo hili aliyezoea kuwatongoza wake za watu alikiona cha mtema kuni wakazi walipomloweshwa maji chafu kisha wakatisha kumvua nguo zote.

Wakazi waliamua kumwadhibu jamaa huyo baada ya juhudi za kumtaka akomeshe tabia yake kugonga mwamba.

“Jamaa huyo anajulikana eneo hili kwa tabia yake ya kuwatongoza mabinti na wake za watu kila wakati tabia ambayo iliwakera sana wakazi,” alisema mdokezi.

Majirani wake wanaume walimuonya aache uhusiano wake wa kimapenzi na wake za watu na wasichana wenye umri mdogo.

Jamaa alikataa kata kata kuwasikiliza jambo lililowafanya waamue kuchukua hatua na kumpa funzo ambalo hatasahau maishani mwake,” aliongeza mdokezi.

Mambo yalimpasukia jamaa hivi majuzi jirani yake alipomfumania akiwa na binti yake kwenye kilabu wakiendelea kubugia pombe.

Inasemekana jirani huyo alimnyanyua jamaa kitini na kumlazimisha waende nyuma ya kilabu huku akimwamuru bintiye kwenda nyumbani mara moja. Jirani kwa hasira alianza kumfokea jamaa vikali akimlaumu kwa kumharibu msichana wake.

“Mwanamume mzima kama wewe hauna haya kuhusisha msichana wangu mwenye umri mdogo kwenye mapenzi na zaidi ya hayo unamfunza kunywa pombe. Nilipata fununu kwamba huwa unamtongoza binti yangu na nimejionea. Leo utakiona,” mzee aliapa.

Jirani huyo aliungana na wakazi kumlowesha jamaa maji chafu yaliyokuwa nyuma ya hoteli na kuita vijana ambao walitisha kumvua nguo lakini akaponyoka na kukimbia akaacha gari lake.

“Wakazi walisikika wakishangilia wakisema kwamba walikuwa wamechoshwa na tabia yake,” alisema mdokezi.

“Hii ni funzo kwa wanaume wote walio na tabia ya kuwaharibia watu wake na binti zao. Ni tabia ambayo hatutakubali hapa kwetu,” mzee mmoja alisikika akisema.