Dondoo

Polo ala rungu kumezea binamuye

August 17th, 2019 1 min read

Na LEAH MAKENA

GATUNGA, THARAKA NITHI

JAMAA wa hapa aliona kilichomnyonyoa kanga manyoya alipoingizwa kwenye gunia na kupokezwa kichapo kwa kujaribu kutongoza binamu yake.

Jamaa alikuwa amepata jiko ila akashindwa kutunza ndoa yake na kumfurusha mkewe akidai warembo wa kuoa walikuwa wengi kama samaki wa baharini.

“Alimfanyia mkewe dharau kubwa kwa kumfukuza mchana akisema kuna wanawake wengi wa kuoa. Hakuweza kutulizwa na yeyote kwa sababu alionya wakazi kutoingilia masuala ya familia yake, ” akasema mdokezi.

Baada ya muda wa siku chache alianza kuonekana na vichuna wa mtaani waliomhepa baada ya kusikia kwamba alimtema mkewe.

“Kila mwanadada aliyemrushia chambo na kuimeza alimuacha baada ya kusikia alivyomtendea mkewe,” alieleza mdokezi.

Hivi majuzi, jamaa aliripotiwa na binamu yake kwa wazee kutokana na tabia yake ya kumtumia jumbe za mapenzi akidai alitaka kumuoa.

Licha ya dada kumuonya kuwa walikuwa na uhusiano wa kifamilia na kumtaka kukomesha tabia hiyo, jamaa aliendelea kurusha mistari na kumuudhi hata zaidi.

Binti aliwasilisha kesi kwa mjomba ambaye aliamua kutoa funzo kwa kijana wake kupitia baraza la wazee.

Baada ya kutafuta watu wenye miraba minne wa kumnyorosha, jamaa aliitwa na kupewa kichapo cha mbwa kabla ya kuelezwa makosa yake.

Huo ndio uliokuwa mwisho wake kuchezea binamu yake huku akisalia kuuguza majeraha na kuapa kuhama mtaani kwa kuwa kicheko kwa wengi.

Inasemekana kuwa wazee waliapa kumchukulia hatua kali zaidi wakipata habari kama hizo tena wakisema alikuwa akiabisha familia na ukoo wao.