Dondoo

Polo alilia mke aliyemzaba kofi

September 28th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

Na KYUU, TAVETA

POLO mmoja kutoka hapa alijipata pabaya alipozabwa kofi na demu waliyeachana kwa kumtaka warudiane. Inaelezwa kuwa polo alikuwa mzembe kupita kiasi huku demu akijikaza kisabuni kujenga boma.

“Polo hupenda sana kunywa pombe mchana kutwa na kutangatanga mtaani.Polo alikuwa akijivuna akisema alikuwa na mke mwenye bidii ya mchwa na hata akishinda mtaani alikuwa akipata kila kitu nyumbani kikiwa shwari,” alieleza mdokezi.

Demu hakupendezwa na tabia ya mumewe kisha akachukua hatua na kurudi kwa wazazi wake.

“Mkewe hakuweza kuvumilia tabia ya jamaa na akarudi kwa wazazi wake. Jamaa alianza kuhangaika baada ya kuachwa pweke,” alieleza mdokezi.

Siku ya tukio, polo na demu walikutana njiani kisha polo akamsimamisha demu na kumwambia kuwa angetaka warudiane.

“Beb, nataka turudiane.Kuanzia leo nitakuwa mchapa kazi.Naomba unisamehe,” polo aliomba. Demu alipuuza maneno ya polo kisha akamrukia na kumzaba kofi moto.

“Sina haja na wewe tena.Unataka kurudiana na nani? Na kwa taarifa yako, siku nyingine ukinisimamisha njiani utanitambua,” demu alimwambia polo. Demu aliondoka na kumuacha polo njiani huku wapita njia wakiangua vicheko kwa tukio hilo.

Baadhi walisikika wakisema jamaa alistahili kichapo hicho huku wengine wakimlaumu mwanadada kwa kudharau mumewe.

“Hata kama anamchukia, hakufaa kumpiga kwa sababu jamaa amewasilisha ombi lake kwa unyenyekevu. Huyo mwanadada ni mbaya, amekosea kuonyesha ujimbi wake hadharani,” alisema jombi mmoja.

Kwa upande wake jamaa alisimama na kuapa kumtafuta mwanadada huyo ili ajue anampenda.

“Nyinyi hamfai kulalamika kwa sababu huyo ni mke wangu na hakunipiga kwa sababu ya kunichukia, ni kwa sababu ananipenda na tabia yangu ni mbaya,” alisema na kwenda zake.