Dondoo

Polo aliyehepa na Sh400,000 za mwanasiasa sasa ni mfugo wa ‘mumama’

January 23rd, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

POLO mwanasiasa wa Kaunti ya Murang’a kwa sasa ako uhamishoni kwa jirani mama mzee baada ya kukopa na akaishia kupigwa mnada.

Akiwa analilia kwa choo, sasa anasikika akiteta vikali kwa mabaa kuhusu vile wanasiasa aliojihusisha nao awali wamemtelekeza katika masaibu yake ya sasa.

“Mimi niliwafanyia kampeni kwa roho safi na kwa bidii yangu yote mpaka wakashinda viti. Waliniahidi kwamba wangenishikilia nianze biashara. Sasa maisha yangu yamevurugika,” akasikika akiteta.

Shida za polo zilianza kujiunda kama wingu la janga wakati alihama kutoka Kambi ya mwanasiasa mmoja na akaruka kwa mwingine akiwa na deni la Sh400,000.

Alikuwa amekopeshwa hela hizo na mwanasiasa huyo kutoka kwa hazina ya maendeleo mashinani lakini akaruka hadi kwa mwanasiasa mwingine kabla hajarejesha pesa hizo.

“Ujanja wa polo ulikuwa alipiwe mkopo huo na mwanasiasa huyo mpya. Tamaa ya kukosa kulipa mkopo ndiyo ilimwongoza. Akasahau wanasiasa ni sawa na wakora wa kufaana,” akasema mdokezi wetu.

Hatimaye, wanasiasa hao wawili walijadiliana na ndipo polo alijipata kwa mataa.

“Mwanasiasa huyo wa kambi mpya licha ya kumwahidi polo angemlipia hela hizo alimruka na akashirikiana kumsaka ili apigwe mnada,” akasema mdokezi.

Polo alishangaa asubuhi kuona magari ya kumchota mali yamefika langoni kwake na ilibidi mke wake na watoto wawili watoroke na kumwachia aibu yake.

“Kwa sasa jamaa wa watu hana mke, hana kwake na hana hela. Masaibu kwake ni kama kivuli chake kumfuatafuata aliko. Lakini bahati kwake ni kwamba kuna ajuza amemhurumia na kumchukua kama mfugo wa mahaba,” akasema mdokezi.

[email protected]