Dondoo

Polo apapura pasta kwa kumvunjia ndoa

October 24th, 2018 1 min read

Na DENNIS SINYO

Bwale, Webuye

KALAMENI wa hapa alimlaumu pasta wa kanisa lake kwa kusambaratisha ndoa yake.

Jamaa huyo na mkewe walikuwa washiriki wakuu wa kanisa la mchungaji huyo kwa muda mrefu kabla ya mambo kwenda kombo.

Inasemekana pasta alianza kumezea mate mke wa jamaa hali ambayo ilisababisha ndoa yao kuanza kuyumba. Kulingana na jamaa, pasta alianza kueneza fitina kila mahali akisema yeye alikuwa mume bwege.

Jamaa alilalamika kwamba mkewe alianza kumdharau akifuata ushauri wa mchungaji huyo.

Kalameni alikasirika kuwa pasta alikuwa akishinda na mke wake masaa mengi akimshauri na wakati mwingine alikuwa akirejea nyumbani usiku.

Baadaye aligundua kwamba pasta alikuwa amemshauri mkewe kumuacha. Jamaa hakuamini kwamba mtu anayestahili kuunganisha wanandoa alikuwa akichochea ndoa yake ivunjike. “Huyu ni mchungaji wa aina gani anayepanga kuvunja ndoa yangu?” aliteta.

Inaarifiwa mama alikuwa amefanya uamuzi wa kuachana na mumewe baada ya kushauriwa na mchungaji.

Majuzi, jamaa alirejea nyumbani na kupata mkewe alikuwa ameondoka na virago vyake.Baada ya uchunguzi, aligundua kwamba pasta alikuwa amempangishia chumba mjini.

Bila kupoteza muda, alienda kumtafuta mchungaji na kumfokea. “Wewe ni mtu wa kuwapa wanandoa mwelekeo, mbona unageuka kuwa tisho kwa ndoa zetu? Umeniharibia ndoa yangu ya miaka mingi. Ninataka kujua umeficha wapi mke wangu?” aliteta jamaa.

Mke wa mchungaji aliyekuwa jikoni alisikia kelele hizo na akamtaka mhubiri kusema ukweli.

Inasemekana mchungaji alikana kufahamu aliko mkewe jamaa. Hata hivyo, jamaa aliapa kumuanika pasta ili watu wafahamu ni kwa hatari wa ndoa zao.