Polo aporwa na kisura ‘malaika’

Polo aporwa na kisura ‘malaika’

Na JOHN MUTUKU SAMUEL

HURLINGHAM, NAIROBI

POLO alibaki kulia na kuomboleza kama mfiwa, akashindwa kutoka nje ya nyumba kichuna aliyemteka kwa ukarimu na urembo wake alipomuacha bila chochote.

Jamaa alipokutana na mwanadada huyo hakufikiria anaweza kuwa hatari.

Polo alihamia mtaani hapa majuzi baada ya kupata kazi yenye donge nono. Alipohamia mtaani, alikutana na kichuna aliyemdokezea aliishi karibu naye. Kichuna ndiye alimsaidia kupanga vitu katika nyumba, kazi ambayo polo hakuipenda.

“Jamani sijui ingekuwaje iwapo usingetokea kunisaidia. Miye sijui kupanga vyombo vya nyumba,” polo alishukuru.

“Usijali. Nipo kwa ajili yako. Bado napanga kukuletea maua bandia nikupangie huku na kule ila siwezi kwa kuwa sina ufunguo,” kichuna alisema.

“Ufunguo huu hapa darling. Kila upatapo nafasi, kuwa huru kuingia humu mwangu,” polo alimhakikishia akimkabidhi ufunguo.

Siku iliyofuata polo alipoenda kazini, kichuna alifika na vijana wake wanne.

Walichukua kila kitu cha thamani katika nyumba hiyo, wakapakia katika lori kisha wakaondoka.

“Mshenzi mkubwa huyo. Atokapo kazini atakuta atakayokuta,” kichuna alisemea akiondoka.

Polo alipokuta nyumba ikiwa tupu, alijiinamia na kulia sana.

“Laiti nisingalimkaribisha kwangu huyo mwanadada, haya yote yasingalinikuta. Hata hivyo, yaliyomwagika hayazoleki. Itabidi nisadiki nishatapeliwa na kichuna na nafaa kuwa makini,” polo alijiliwaza baada ya kuelezea majirani yaliyotendeka.

Tangu siku hiyo, polo hapumbazwi na urembo wa mademu. Ameamua akitamani mke, itabidi amtafute kwa uangalifu.

“Haufai kuamini mwanadada yeyote hii Kanairo. Ona sasa umepoteza mali kwa kuamini demu ambaye alijifanya malaika kwako ilhali humjui wala anakoishi,” jirani mmoja alimweleza jamaa.

You can share this post!

WARUI: Mfumo wa CBC ni mzigo kutokana na ughali wa vifaa

Siku 365 za kufa kupona