Dondoo

Polo atimuliwa na mahari yake ya kuku

August 7th, 2018 1 min read

Na LEAH MAKENA

Irunduni, Tharaka

POLO wa hapa nusura achapwe na mashemeji alipowapelekea kuku wawili kama mahari siku chache baada ya kuhepa na dada yao.

Yasemekana jamaa alikuwa akimchumbia mwanadada huyo kwa muda licha ya pingamizi kutoka kwa ndugu zake.

Kulingana na mdokezi, ndugu za mwanadada huyo walikuwa wameshindwa kumshawishi dada yao kumtema polo wakidai kwamba alikuwa mlala hoi.

“Mwanadada alitia masikio nta na kuhamia kwa polo licha ya kukatazwa na ndugu zake. Juhudi za kuwasiliana naye ziligonga mwamba alipozima simu,” alisema mdokezi.

Wiki moja baada ya kuona kuwa amefaulu kukaa na mrembo, ndipo polo alifika nyumbani na alipopata wazazi, akawa na muda wa kujitetea na kueleza sababu ya kuhepa na binti yao.

“Naomba mniwie radhi kwa sababu sikuwa na uwezo wa kuandaa karamu kubwa wala kufanya harusi. Ninaahidi kutia bidii angaa nipate cha kuwatunuku huku nikihakikisha kuwa binti yenu anakula na kuvaa vizuri,” polo alijitetea huku akiwataka wazazi kupokea kuku aliokuwa amebeba.

Duru zasema kuwa mashemeji walivutiwa waya na wakalazika kuacha vinywaji klabuni kwenda kumkabili polo.

Mkutano wa jamaa na wakwe ulikatizwa na mashemeji walipofika kwa fujo na kujaribu kumtia polo viganjani ila wakashindwa alitimua mbio na kutokomea.

“Unadhani unayedai kuwa mkeo ameokotwa ndipo ulete mahari ya kuku?Umetupa mbao kutonesha kidonda kwani tunakuhakikishia kuwa hutaishi naye kabisa,” ndugu wa mwanadada waliteta.

Habari zasema kuwa mashemeji walibeba kuku hao tayari kuwarudisha kwa polo huku wakiapa kumtwaa dada ili warudi naye nyumbani na kutishia kumkomesha iwapo angeendelea kuwa kero kwao.

…WAZO BONZO…