Dondoo

Polo atishia kuroga demu kwa kumtema

November 1st, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

Kawangware, Nairobi

KIOJA kilizuka kwenye ploti moja mtaani humu baada ya polo kutisha kumroga mrembo aliyemtema

Inadaiwa polo alitishia kumpeleka mrembo kwa mganga ili apewe adabu kwa kukatalia mali yake baada ya kutimuliwa.

Duru zinaarifu kwamba mrembo aliamua kumtimua polo huku akimuonya kutokanyaga kwake tena akidai muda wa kuishi naye ulikuwa umekamilika.

Penyenye zinasema wawili hao walipokuwa wakichumbiana, mrembo alimshawishi polo kuacha nyumba yake na kuhamia kwake.

Wenyeji walishangazwa na namna polo alivyotimuliwa. “Huyu jamaa ni mjinga sana. Anawezaje kuhamia nyumba ya mrembo! Sasa amefukuzwa kama mbwa,” wenyeji walishangaa.

Inasemekana kabla ya kuondoka, polo alitaka apewe vitu alivyokuwa amenunua alipokuwa akiishi na kipusa.

“Nataka unipe kiti, kitanda na meza. Ni mimi niliyevinunua,” polo alimueleza mrembo.

Inasemekana mrembo alimkaripia huku akitishia kumuitia polisi. “Nilipohamia kwako ulikuwa ukilala chini. Chakula unalia mekoni kwa vile haukuwa na meza. Lazima unipe mali yangu,” polo aliapa.

Mrembo hakushughulika. Aliamua kuufunga mlango na kumueleza jamaa kuondoka.

“Tutaona nani atakayecheka wa mwisho. Hauwezi kunifukuza na ubaki na mali yangu,” jamaa alisema.

Mrembo hakushtuliwa na maneno ya polo. “Umeamua kunitoa kwako kwa njia ya aibu. Tena unakatalia mali yangu. Walahi nitakupeleka kwa mganga. Vyangu haviendi bure,” polo aliapa.

Inadaiwa mrembo aliposikia neno mganga, alimueleza polo aingie chumbani atoe kilichokuwa chake.

“Ungekataa na vitu vyangu ungejua mimi ni nani. Kama ni nyasi ungezitafuna. Cheza na mimi utakiona,” polo alitishia.

Mrembo alibaki kimya huku jamaa akiendelea kupanga vitu vyake.

“Chezea mtu mwingine lakini si mimi. Boma letu nyumbani tumezingirwa na waganga. Na wote ni mambo mbaya,” polo alizidi kumtishia.