Dondoo

Kalameni atiwa adabu kukwepa kulipia danguro

May 30th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KAWANGWARE, NAIROBI

Wapangaji kwenye ploti moja mtaani humu walitazama sinema ya bure baada ya polo kupewa viboko vikali kwa kukataa kulipa ada ya chumba alichotumia kama danguro.

Inadaiwa polo alifika kwa jamaa anayeishi hapa akiwa na mpango kwa kando na kuomba chumba ili aweze kuchovya asali.

“Niaje boss. Huyu ni demu wangu. Hatujaonana naye kwa muda mrefu. Nataka unipe nafasi hapa kwako kwa dakika chache kisha aende,” polo alimueleza jamaa.

Inasemekana jamaa alikubali kumpa polo chumba lakini kwa sharti kwamba angelipia muda ambao angechukua hapo na gharama ya usafi wa malazi.

“Hii nyumba nalipa renti. Godoro na blanketi lazima nitafute mtu wa kuosha. Lazima utoe ada kidogo,” jamaa alimueleza polo.

Duru zinasema kwamba wawili hao walikubaliana. Jamaa aliondoka na kumuacha polo pamoja na kimada wake kwa nyumba.

Penyenye zinasema kwamba jamaa alikuwa akijulikana sana kutokana na tabia ya kuwapa makalameni chumba chake kwa matumizi ya kuwashughulikia mipango ya kando.

Inadaiwa saa mbili zilipita na polo hukuonesha dalili za kutoka. Jamaa aliamua kumpigia simu huku akimuarifu kuwa muda wake ulikuwa umeisha.

“Muda huu wote unafaa kunilipa pesa nzuri. Hebu nipe Sh1000,” jamaa alimueleza polo.

Polo alitoa Sh200 huku akiahidi kutuma zilizosalia baadaye. “Hakuna kitu kama hicho. Wewe tunamalizana sasa hivi,” jamaa alidai.

Polo alibaki asijue la kufanya. “Kama ulijua huna pesa basi ungempeleka mrembo wako kwako ama mfanyie mambo yenu kwa msitu. Weka pesa hapa,” jamaa alifoka.

Mrembo aliamua kuchomoka mbio. “Wewe huondoki hapa. Ulipoingia hapa tulikubaliana. Malazi lazima nioshe. Leta pesa zote,” jamaa alimfokea polo.

Wapangaji kwenye ploti walianza kukusanyika huku wakitaka kujua kilichokuwa kikiendelea. Inadaiwa jamaa alichomoa kiboko na kuanza kumwangushia polo.

“Ujinga wako peleka kwenu. Hakuna vya bure hapa,” jamaa alimkaripia polo.