Dondoo

Polo mpenda sketi ajuta kugeuza nyumba ya nduguye kuwa danguro

October 19th, 2018 1 min read

Na DENNIS SINYO

Cherangany, Trans Nzoia

JOMBI mmoja alijipata mashakani ndugu yake alipomlaumu kwa kugeuza nyumba yake mpya kuwa danguro.

Yasemekana jamaa alihamia nyumba ya ndugu yake mkubwa wiki moja baada ya ujenzi kumalizika.

“Siku chache tu baada ya nyumba hiyo kupakwa rangi, jamaa huyo alibeba virago vyake na kuhamia hapo bila kuomba ruhusa kutoka kwa ndugu yake,” alieleza mdaku wetu.

Penyenye zasema jamaa hakuwa amemwambia yeyote kwamba alikuwa akihamia kwenye nyumba hiyo ya kifahari.

Aligeuza nyumba hiyo kuwa makazi ya vidosho wa kila aina. Kila siku, vipusa tofauti tofauti walikuwa wakionekana wakiingia na kutoka kwenye nyumba hiyo.

“Jamaa aligeuza nyumba ya nduguye kuwa danguro na kujiburudisha na akina dada hao,wengine wakipiga kambi kwa siku kadhaa.Tukio hilo halikuwafurahisha watu wa familia na majirani,” alieleza mdokezi.

Mamake alimuonya aache kuleta wasichana kwa nyumba ya nduguye lakini hakusikia hadi vipusa wawili walipokatalia katika nyumba hiyo.

Aliposikia kwamba vipusa walikuwa wamekatalia katika nyumba yake, mwenye nyumba alifika na kumkashifu jamaa kwa kutia najisi nyumba yake.

Jamaa alilaumiwa pakubwa kwa kuzama kwenye anasa na kukosa mwelekeo. Aliagizwa kubeba kila kitu chake na kuhama nyumba hiyo mara moja.

Wasichana hao hawakuamini kuona jamaa akifurushwa kama mahabusu kutoka kwenye nyumba hiyo.

“Mwanaume mzima anaringia wasichana na kumbe nyumba si yake. Sasa amefukuzwa mchana kutwa jamani, ”alisema jirani mmoja.

Iliwabidi akina dada hao kuondoka wakimfuata jamaa unyo unyo. Hata hivyo, walibadilisha mawazo yao na kuabiri piki piki kwenda mjini huku jamaa akirejea kwenye kibanda chake cha zamani.