Habari za Kaunti

Pombe: Hoteli 5 zafungwa msako ukiendelea

March 28th, 2024 1 min read

NA STEPHEN MUNYIRI

HOTELI tano za hadhi mjini Karatina, Kaunti ya Nyeri, zilifungwa Jumatano baada ya Rais William Ruto kuzuru kaunti hiyo na kusema serikali haitalegeza kamba katika kupambana na pombe haramu.

Wakati ambapo operesheni dhidi ya pombe haramu na mihadarati imekuwa ikiendelea, hoteli hizo zilisazwa. Wamiliki wao sasa wanalalamika kuwa kufungwa kwao kutaathiri shughuli za kitalii hasa wakati huu wa likizo ya Pasaka ambapo wao huwapokea wageni wengi.

Hoteli zilizofungwa ni Starbucks, Omega Gardens, Oldoiyo, Ibis, Seven Eleven Lounge na Derby Place.

Zinadaiwa ziko karibu na kanisa, shule na makazi.

Msako wa kumaliza pombe haramu umekuwa ukiendelezwa Karatina ambapo ni nyumbani kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Karatina imekuwa na zaidi ya mabaa 400 ambazo zipo karibu na shule na makanisa.

Hata hivyo, Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga amesema operesheni hiyo inalenga kusambaratisha biashara za watu na imekuwa ikiendelezwa kwa mapendeleo.

“Nimeuliza Kamishina wa kaunti kwa nini oparesheni hii inaendelezwa Mathira pekee na si maeneo mengine ya kaunti. Wafanyabiashara hawa walienda kortini na kupata amri ya kutofuta leseni zao na inashangaza sasa kuwa biashara zao zinafungwa,” akasema Bw Wamatinga baada ya kukutana na mamia ya wanaoendesha biashara ya baa.

Hata hivyo, Kamishina wa Nyeri Pius Murugu alikanusha madai ya Bw Wamatinga akisema kuwa serikali haibagui yeyote katika kutekeleza operesheni dhidi ya pombe haramu.