Habari Mseto

Pombe ya mnazi si haramu hivyo wagema walindwe, Mbunge aambia Kindiki

April 6th, 2024 2 min read

Na WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya amemtaka Waziri wa Usalama Bw Kithure Kindiki kuweka bayana suala la vita dhidi ya pombe haramu nchini, akidai kuwa mnazi ambacho ni kinywaji kinachotumiwa na jamii ya Mijikenda kitamaduni si haramu na kinasaidia familia nyingi.

Bw Baya alimwandikia barua Prof Kindiki na wakuu wa usalama eneo la Pwani akiwataka kuhakikisha wauzaji wa mnazi hawahangaishwi na maafisa wa polisi.

Mbunge huyo, alisema vita dhidi ya pombe haramu vimewanasa wakulima wa nazi, wagema, watengenezaji na wauzaji wa kileo hicho.

Hata hivyo alisema viongozi wa Pwani wataendelea kupinga vikali kuharamishwa kwa mvinyo huo unaotokana na mmea wa nazi.

Bw Baya alisema kwa zaidi ya miaka 20, watengenezaji na wauzaji wa mnazi wamekuwa wakifanya biashara zao bila changamoto yoyote.

“Hata hivyo tangu serikali ianzishe vita dhidi ya pombe haramu hivi majuzi ulanguzi wa dawa za kulevya na uraibu sugu wa vileo jamii zinazojihusisha na mnazi zimeathirika,” alifichua Bw Baya.

Alisema wakulima ambao hutengeneza na kuuza mnazi wanahangaishwa na maafisa wa polisi.

Alisema kwa mujibu wa kipengele cha sheria ya Udhibiti wa Pombe 2010, pombe ya mnazi haijaharamishwa.

“Sababu mnazi ni kinywaji cha kitamaduni na kidini ambayo inapendwa na wapwani na hata watalii. Mnazi si pombe haramu. Lazima tuheshimu tamaduni zetu,” alisema Bw Baya.

Aidha aliitaka serikali kuu kutoingilia maswala ya kitamaduni akitaja kuendelezwa kwa misako dhidi ya mvinyo huo kulenga kuhujumu uchumi wa Pwani.

Aliuliza kwanini serikali haipambani na mugukaa au miraa ambayo imetajwa kuwa miongoni mwa dawa za kulevya.

“Mbona miraa na mugukaa inaheshimiwa na serikali? Tunataka mnazi pia upewe heshima yake ili wakulima na wauzaji waendelee na biashara zao,” alisema akiongeza kuwa mnazi unafaa kupata soko nchini.

Vile vile aliisihi serikali kuu kuwahamasisha wakulima wa mnazi ili kukuza zao hilo linalowapatia matapo mazuri kuinua uchumi wa Pwani.

Bw Baya aliitaka serikali kufanya kikao na washikadau wa sekta hiyo ili kujua umuhimu wa mnazi kwa jamii ya mijikenda.

Haya yanajiri wiki chache baada ya Gavana Bw Gideon Mung’aro, Spika wa Bunge la kaunti hiyo Bw Teddy Mwambire na viongozi wengine wa kaunti hiyo kuapa kupiga marufuku miraa na muguka endapo serikali itaendelea kuhangaisha wauzaji wa mnazi.