Pombe ya mnazi yaleta dhuluma kwa wasichana

Pombe ya mnazi yaleta dhuluma kwa wasichana

Na MAUREEN ONGALA

WATETEZI wa haki za watoto Pwani wameeleza wasiwasi kuhusu dhuluma zinazotekelezwa dhidi ya wasichana katika maeneo ya kuuza pombe ya mnazi, maarufu kama ‘mangwe’.

Biashara ya pombe hiyo imevutia kina mama wengi Kilifi, ambao huchukua mvinyo kwa mkopo kutoka kwa wagema kisha kulipia baadaye.Dhuluma hizo dhidi ya wasichana wadogo zinaaminika kutokana na jinsi baadhi ya wanawake hao, hulazimika kugeuza maboma yao kuwa mangwe kwa kukosa fedha za kukodisha sehemu mahususi za kibiashara kuuzia pombe hiyo.

Mzee wa kijiji cha Mabirikani viungani mwa mji wa Kilifi, Bi Aisha Saidi, alisema wengi wa wamama wanaouza mnazi ni wajane, ama walioachana na mabwana zao kwa sababu mbalimbali za kinyumbani.“Biashara hii imekuwa hatari sasa.

Kila tunapokataza akina mama kufanya biashara hii katika nyumba zao, wanatuambia tuwape njia mbadala ya kupata riziki na kulea watoto wao. Huwa wanatushtaki kwa wanasiasa ambao hutusuta,” akasema.Kulingana na Bi Saidi, lalama za wanawake hao zinaeleweka kwani wengi ni maskini;

ila viongozi wa kisiasa wangekuwa mstari wa mbele kutambua hatari iliyopo kwa watoto, na kuwasaidia kuboresha biashara hizo ziwe mbali na maboma yao badala ya kusuta wanaharakati wanatoa tahadhari.“Ni muhimu wafanye biashara yao wakizangitia sheria na afya pamoja na kuwalinda watoto.

Ni jukumu la machifu na wazee wa mitaa kuhakikisha hakuna mtoto atapatikana katika maeneo hayo,” akasema.Kitongoji cha Kisumu Ndogo mjini Kilifi ni mojawapo ya maeneo yanayojulikana kwa idadi kubwa ya mangwe zilizofunguliwa kiharamu.

Katika mtaa huo, utakutana na vibanda vidogovidogo vichafu vilivyojengwa kwa magunia yaliyozeeka, mifuko ya simiti iliyotumika na karatasi za nailoni katikati ya makazi ya watu.Mangwe hizi hufunguliwa kila siku kwa saa 24 zikipiga muziki wa juu, huku walevi wakipiga kelele na kuongea lugha chafu na matusi mazito licha ya watoto kupitia hapo.

Hakuna choo wala jaa la kutupa taka, na mara kwa mara walevi huenda haja ndogo kando ya barabara na kwenye kuta za nyumba za watu.Taifa Leo ilibaini kuwa, baadhi ya wanawake wanaouza mnazi hushinda na watoto wao mangweni kuwasaidia kuhudumia wateja, badala ya wanafunzi hao kwenda shule.

Ni katika kukurukakara za kuosha mirija, vikombe na chupa za walevi au hata kupeleka vinywaji mezani, ndipo wasichana huanza kudhulumiwa. Afisa wa Miradi katika shirika Center for Rights Awareness Education (CREAW) Kaunti ya Kilifi, Bi Faith Tsuma, alisema inahofiwa kuwa dhuluma za ngono ziliongezeka wakati shule zilipofungwa mwaka jana humu nchini, kufuatia mkurupuko wa janga la virusi vya corona.

Utafiti wa awali uliofanywa na shirika hilo mnamo 2017 ulidhihirisha kuwa, wasichana wadogo ambao ni wahudumu katika mangwe hizo hupitia dhuluma za ngono miongoni mwa changamoto zingine.“Kuna wateja maalum ambao wamama hawa huwathamini. Huwakabidhi wanaume hao mabinti wanaowauzia mnazi, ambapo wasichana hao hulazimishwa kushiriki ngono na wateja,” akasema Bi Tsuma.

Kando na hayo, alisema kuwa wanawake wengi wanaouza mnazi hupigwa na wanaume ambao huwa hawataki kulipia pombe waliyokunywa.“Kuna uovu mwingi unaotendeka katika sehemu hizi za kuuza mnazi licha ya kuwa watu hujumuika hapo kujivinjari,” akasema.Katika mahojiano, Kamshina wa Kaunti ya Kilifi, Bw Kustwa Olaka alikiri kuwa idadi kubwa ya mangwe eneo hilo ni suala linaloibua wasiwasi kuhusu usalama.

Alieleza kwamba imekuwa vigumu kupiga marufuku biashara ya mnazi kwa vile ni tegemeo la pekee kwa idadi kubwa ya wamama maskini.Hata hivyo alisema mashirika mbalimbali ya serikali ya yasiyo ya kiserikali yameungana kutoa hamasa kuhusu hitaji la kulinda watoto na kutii sheria hata biashara hizo zinapoendelezwa.

Afisa mkuu wa afya ya umma, Bw Erick Maitha alisema kila mfanyibiashara wa chakula au mvinyo anastahili kuwa na stakabadhi ya afya na kufanya biashara yake mahali panaporuhusiwa kisheria.Mmoja wa wakazi, Bi Mercy Nyambu alisema kuwa juhudi zao kupitia serikali ya kaunti na kitaifa kutaka mangwe hizo kuondelewa katika sehemu za makazi hazijafua dafu.

“Tunaishi maisha ya hatari sana na kila mara tukitafuta usaidizi tunaambiwa kuwa hakuna sheria ya kusimamia biashara ya mnazi,” akasema.

You can share this post!

Magavana mbioni kukamilisha miradi kabla ya kustaafu

Gavana apongeza hatua za kufufua sekta ya korosho

T L