Makala

Pomegranate hukuzwa kurembesha mazingira ingawa matunda yake yana manufaa tele kiafya

April 26th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

UKIZURU kiunga cha Catherine Nyokabi kilichoko Laikipia Mashariki, katika mazingira ya lango utalakiwa na miti yenye mvuto na umaridadi wa aina yake.

Wakati wa ziara ya Taifa Leo Digitali, tulikaribishwa na miti iliyojipamba kwa matunda ya rangi nyekundu na kahawia.

Mkulima na mtaalamu huyu wa kilimo amepanda miti kadhaa ya Pomegranates. Ni aina ya mimea inayopandwa katika mazingira kwa minajili ya kuyarembesha kutokana na rangi yake maridadi ya maua yanapochana na matunda. Kimaumbile, yanafanana na matufaha.

Aidha, matunda haya ni kiini kizuri cha Fibre, Vitamini A, C, B na K. Pia yamesheheni madini ya Calcium, Potassium na Iron.

Mbali na urembesho wake, kwa sababu ya tija zake kiafya yanakuzwa kwa wingi Bara Uropa na Asia.

Mataifa mengine yanayoyapanda ni Persia, Babylonia, Iran na India. Afrika, Misri ndiyo inajulikana kuyakuza.

Bi Catherine Nyokabi anasema hakuyapanda kwa ajili ya umaridadi pekee, ili kwa sababu ya faida zake kiafya pia.

“Ni kitega uchumi changu. Nina wateja wanaoyanunua kwa sababu ya manufaa yake kiafya,” adokeza.

Bi Catherine Nyokabi, akionyesha matunda aina ya pomegranates. Picha/ Sammy Waweru

Kulingana na mkulima huyu ni kuwa matunda haya yanastahimili kiangazi.

Yanastawi maeneo yenye baridi kali, chini ya nyuzi -12 sentigredi.

Hata hivyo, Catherine anaeleza kwamba yanafanya vyema na kuzalisha kwa wingi maeneo yanayopokea miale ya jua kwa muda mrefu. Udongo unaotuamisha maji unaathiri ukuaji wake, hivyo basi hayastawi eneo lenye maji mengi, yaani chemichemi.

Udongo bora katika kilimo cha pomegranates ni tifutifu au changarawe.

“Hayana kikwazo cha asidi au alkalini ya udongo. Japo, yanakua vizuri katika udongo wa asidi ya chini,” amasema Bi Catherine.

Kuna njia aina tatu kuyapanda; kutoka kwa mbegu moja kwa moja, miche au matawi. Matunda ya pomegranates yana ukubwa wa duara kati ya inchi 2 hadi 6, kila tunda likikadiriwa kuwa na mbegu 200-1, 400.

Mbegu zake hukaushwa siku kadhaa kabla ya kupandwa. Hata hivyo, Catherine anasema utumiaji wa matawi na miche ndizo njia bora.

Charles Kibugi, mkulima wa pomegranates Nyeri anasema matawi yanapaswa kuwa na urefu wa hadi sentimita 40. Andaa mashimo urefu wa sentimita 50 kuenda chini. Kutoka shimo moja hadi nyingine, nafasi iwe karibu futi 8.

“Upanzi wa matunda haya pia hufanywa kwenye vyungu. Vitiwe udongo uliochanganywa vyema na mbolea, kisha matawi yapandwe,” asema Bw Kibugi. Mkulima huyu anafafanua kwamba sehemu ya chini ya tawi ielekezwe ardhini, hadi sentimita 15 hivi.

Kwa mujibu wa maelezo ya mtaalamu Catherine Nyokabi, ni kuwa matunzo yake ni maji, palizi na kuyalisha kwa njia ya maji na mbolea; asili au fatalaiza. Mbolea yenye ukwasi wa Nitrojini na Potassium, ndiyo bora katika kuongeza kiwango cha mazao.

“Walio maeneo yasiyopokea mvua kwa wingi, watumie mfumo wa kunyunyizia mimea maji kwa mifereji,” anashauri.

Ni muhimu kupogoa (pruning) matawi, ili kupata mazao bora, kulingana na mdau huyu. Pia, matawi yanayopogolewa ni yaliyoharibika na kuathiriwa na wadudu.

Wadudu wanaoyashambulia ni vidukari na vipepeo. Magonjwa kwa matunda haya ni nadra kushuhudiwa. Ili kudhibiti wadudu, mkulima anahimizwa kutafuta ushauri kutoka kwa mtaalamu ili kuelekezwa dawa maalum.

Pomegranates huanza kuzaa matunda miaka mitatu baada ya upanzi. Mtu uliokomaa huzalisha zaidi ya matunda 100 kwa mwaka. Tunda moja hugharimu kati ya Sh50 hadi Sh200.

Ekari moja inaweza kusitiri karibu miti 300 ya pomegranates. Wanaokuza miche yake, huuza zaidi ya Sh200, mmoja.