Habari Mseto

Pondeni raha mkijua Januari ni shule – Magoha

December 6th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, amewataka wazazi wajiandae kwa ufunguzi wa shule Januari 2021 hata wanapoendeleza mipango ya kusherehekea sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya.

Akizungumza Jumamosi alipozuru shule ya msingi ya Kamenu mjini Thika ili kujionea mipango inayoendeshwa huko, Prof Magoha alisema shule zote za msingi na za upili ni sharti zifunguliwe Januari 4, 2021, jinsi ilivyopangwa na serikali.

“Wazazi wanastahili kujitayarisha vilivyo kwa sababu wanafunzi wamekaa nyumbani kwa muda mrefu kutokana na janga la corona,” alisema Prof Magoha.

Baadhi ya wadau, wakiwemo viongozi wa kidini tayari wameanza kutoa wito ufunguzi wa shule uahirishwe tena.

Sababu zao ni kwamba, pangalipo hatari ya maambukizi ya virusi vya corona na pia wazazi wengi bado hawana uwezo wa kujimudu kifedha.

Wakati huo huo, Prof Magoha alisema madawati ya shule yatasambazwa katika shule za msingi zilizo Thika Magharibi kabla ya mwezi Disemba kukamilika.

Alisema tayari madawati 400 yamesambazwa katika shule chache eneo la Thika Maghjaribi, huku mengine 300 yakitarajiwa kupelekwa katika shule hizo baadaye.

Alisema wizara ya elimu tayari imelipa mafundi wote waliokamilisha kazi zao na kuwasilisha madawati hayo mahali panapostahili.

“Tayari nimezunguka katika shule kadhaa hapa nchini na nimeridhika na jinsi matayarisho yanavyoendeshwa na walimu wakuu,” alisema Prof Magoha.