Michezo

Pongezi kwa Kariobangi Sharks kushinda Kombe la Ngao ya FKF

October 25th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

RAIS wa Shirikisho la soka nchini(FKF) Nick Mwendwa ameipongeza timu ya Kariobangi Sharks kwa kushinda Kombe la ngao ya FKF na kufuzu kushiriki mechi za kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho Barani Afrika msimu ujao, 2018/19.

Kariobangi Sharks Jumamosi Oktoba 20 walishinda ubingwa huo kwa kuwakalifisha mabingwa wa KPL mwaka wa 2009, Sofapaka 3-2 kwenye mechi ya kusisimua ugani MISC Kasarani.

Akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kusheherekehea ushindi huo na kuhudhuriwa na benchi ya kiufundi pamoja na wanasoka wote, Mwendwa ambaye ni mlezi wa timu Kariobangi Sharks aliwataka wachezaji kujiamini na kucheza kwa kujituma michuano ya bara itakapong’oa nanga rasmi ili kuweza kuletea taifa hili sifa kem kem.

Vile vile kiongozi huyo wa FKF alionyesha kuridhishwa na utendakazi wa benchi ya kiufundi inayoongozwa na kocha William Muluya aliyemtaja kama mkufuzi aliyechangia pakubwa ufanisi wa kupigiwa mfano wa timu hiyo katika kipindi kifupi alichohuduma kama kocha wao.

Katika msimu wa KPL mwaka wa 2018/19, Sharks walimaliza katika nafasi ya sita na vile vile wakatoa mfungaji bora wa ligi hiyo Erick Kapaito aliyeyatia wavuni mabao 16 na kuwapiku Elvis Rupia aliyesakatia Nzoia Sugar kabla ya kuyoyomea  ligi ya Zambia ili kuwajibikia timu Power Dynamos na Jacques Tuyisenge anayesakatia mabingwa mara 17 wa KPL Gor Mahia.

Msimu jana,wa 2016/17 Kariobangi Sharks pia walitoa mfungaji bora, Masoud Juma ambaye baadaye aliagana nao na kuenda kusakata soka ya kulipwa nje ya nchi.