Posta Rangers yaipiga Gor Mahia

Posta Rangers yaipiga Gor Mahia

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Gor Mahia wanaendelea kusikitisha mashabiki wao baada ya kupoteza alama tatu kwa mara ya pili mfululizo kwenye Ligi Kuu kufuatia kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Posta Rangers, Jumatano.

Vijana wa kocha Carlos Manuel Vaz Pinto walijibwaga uwanjani wakiuguza kipigo cha magoli 2-0 kutoka kwa KCB mnamo Machi 7. Inamaanisha kuwa mabingwa hao wa mataji 19 ya Ligi Kuu hawana ushindi wala bao katika mechi zao mbili mfululizo za nyumbani. Zote zilisakatiwa uwanjani Moi Kasarani jijini Nairobi.

Katika mchuano wao wa hivi punde, Gor walipata nguvu ya mtu mmoja baada ya beki wao wa zamani Michael Apudo, ambaye alijiunga na Posta majuzi, kulishwa kadi nyekundu kwa vyoga mshambuliaji Tito Okelo ya dakika ya tatu.

Licha ya kuwa wachezaji 11 dhidi ya 10 wa Posta, Gor ilishindwa kutumia ulegevu wa Posta kwa manufaa yake na kuishia kupoteza baada ya kufungwa na Francis Nambute mwisho wa kipindi cha kwanza.

Matokeo haya yanamaanisha kuwa Gor haina ushindi nyumbani katika mechi tatu mfululizo za ligi nyumbani. Ilianza mwezi Februari kwa kutoka 0-0 dhidi ya mahasimu wao wa tangu jadi AFC Leopards (Februari 7) kisha ikapigwa na KCB na Posta.

Ilikuwa pia imepoteza nyumbani dhidi ya NAPSA Stars 1-0 katika mechi ya kuingia makundi ya Kombe la Mashirikisho la Afrika (Confederations Cup) mnamo Februari 14. Imeshinda mechi moja pekee – dhidi ya Kakamega Homeboyz ugenini mnamo Machi 3 – kutoka saba zilizopita.

Kufuatia kipigo dhidi ya Posta, Gor inasalia katika nafasi ya nane kwa alama 19. Imecheza michuano 13. K’Ogalo wako alama 16 nyuma ya viongozi Tusker ambao wamesakata mechi 15. KCB (alama 29), Leopards (28), Bandari (26) na Kariobangi Sharks (25) zinakamilisha orodha ya timu tano za kwanza kwenye ligi hiyo ya klabu 18. Zoo inavuta mkia kwa alama saba baada ya kukamilisha mechi yake ya 13 kwa sare ya 0-0 dhidi ya nambari 15 Vihiga uwanjani Kericho Green. Vihiga ina alama 10.

You can share this post!

Kenya yaandikisha idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya...

Wasiwasi wakulima wa mahindi kugeukia miwa