Michezo

Posta Rangers yalaza Nairobi Stima na kusalia katika ligi kuu

June 20th, 2019 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

POSTA Rangers wataendelea kushiriki kampeni za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu ujao baada ya kuwazidi maarifa Nairobi Stima katika mchujo kwa jumla ya mabao 3-2.

Chini ya kocha John Kamau, Rangers waliambulia Jumatano sare ya 1-1 dhidi ya Stima iliyokuwa ikiwania fursa ya kupanda ngazi kutoka Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Mchuano huo wa marudiano ulichezewa ugani Kenyatta, Machakos.

Rangers waliingia katika mchuano huo wakijivunia hamasa ya kukizamisha chombo cha Stima kwa mabao 2-1 mwishoni mwa wiki jana mjini Mombasa.

Kujaribu tena

Stima ambao kwa sasa wananolewa na kocha Evans Mafuta watalazimika kujaribu bahati ya kufuzu kwa kivumbi cha KPL kwa mara nyingine msimu ujao baada ya kuwa pua na mdomo kufikia ufanisi huo muhula huu.

Rangers walitangulia kuona lango la Stima hapo Jumatano katika dakika ya tatu kupitia kwa Francis Nambute ambaye pia alikuwa mfungaji wa bao la kwanza kabla ya Joackins Atudo kufunga la pili katika mechi ya mkondo wa kwanza.

Goli la Stima mjini Machakos lilifumwa wavuni na Dennis Oalo ambaye kwa sasa anajivunia jumla ya mabao 27 kapuni msimu huu. Oalo ndiye aliyewafuta tena chozi la waajiri wake mjini Naivasha wikendi jana.