Michezo

Presha Arsenal ikikialika kikosi cha Victoria SC

October 24th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

SIKU chache baada ya kuchapwa 1-0 na Sheffield United katika pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugenini, Arsenal watakuwa nyumbani ugani Emirates Stadium leo Alhamisi usiku kujaribu bahati dhidi ya klabu ya Victoria SC ya Ureno kwenye mechi ya Europa League.

Ni mechi ambayo imekuja wakati kocha wao, Unai Emery anakabiliwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki kufuatia kichapo hicho ambacho kiliwanyima fursa ya kujitoza katika nne bora ligini, kwani wanakamata nafasi ya tano kwa mwanya wa pointi mbili, nyuma ya Chelsea.

Kabla ya kichapo hicho, mashabiki walikuwa wameshuhudia timu yao ikiibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Eintracht Frankfurt ya Ujerumani kabla ya kuandikisha matokeo mangine mazuri ya 4-0 dhidi ya Standard Liege 4-0.

Ushindi huo mfululizo uliwapa pointi zote sita katika Kundi F huku Liege na Frankfurt zikifuata, lakini lazima kocha Emery apiganie ushindi leo usiku ili kurejesha mioyo ya mashabiki hao wa Emirates.

Vitoria wanashikilia nafasi ya mwisho katika kundi hilo baada ya kupoteza mechi zote mbili za kwanza dhidi ya Liege na badaye Frankfurt.

Arsenal kwa sasa haina majeraha yoyote makubwa na hivyo kocha hatakuwa na sababu yoyote ya kueleza iwapo watashindwa kuvuma uwanjan. Ni mshambuliaji Alexandre Lacazette anayeuguza jeraha la enka.

Nyota mwingine atakayeikosa mechi hiyo ni Reiss Nelson ambaye aliumia Jumatatu ugani Bramall Lane wakicheza na Sheffield United.

Mabadiliko yatarajiwa kikosini

Hata hivyo, Emery anatarajiwa kufanya mabadiliko kadhaa kikosini ili kuwapa makinda kadhaa kuonyesha uwezo wao dhidi ya Victoria SC.

Emi Martinez anatarajiwa kulinda lango huku mabeki wa katikati wakiwa Rob Holding na Shkodran Mustafi.

Huenda Mesut Ozil akaanza baada ya kupuuzwa walipocheza na Sheffield United pamoja na Emile Smith Rowe na Gabriel Martinelli katika safu ya ushambuliaji.

Hector Bellerin na Kieran Tierney pia wanatarajiwa kuanza baada ya kukosa kucheza dhidi ya Sheffield United Jumatatu usiku, pamoja na Dani Ceballos na Lucas Torreira kimiliki safu ya kiungo.