Michezo

Presha Ingwe ikikabana na miamba Tusker

March 9th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

AFC Leopards ina mtihani mgumu mjini Machakos inapokabiliana na Tusker FC, wakati mashabiki wao watawatarajia kuendeleza matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya majuzi kuandikisha ushindi wa 1-0 dhidi ya Sony Sugar.

Leopards walipata ushindi huo ugani Bukhungu baada ya kucheza mechi sita bila ushindi, na hii ni fursa nyingine kwao kudhihirishia mashabiki wao kwamba matokeo ya Bukhungu hayakuwa ya kubahatisha.

Kwingineko, Western Stima watakuwa Nairobi kupepetana na Mathare United ambao matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa msimu huu yanazidi kuyeyuka.

Mabingwa watetezi wa GOtv, Kariobangi Sharks wamekuwa Machakos dhidi ya Posta Rangers katika mechi iliyoanza saa nane.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Gor Mahia hawajajumuishwa kwenye ratiba ya wikendi hii kutokana na pambano lao la kimataifa nchini Misri ambapo wamepangiwa kucheza na Zamalek katika mechi ya CAF Confederation Cup, kesho, Jumapili.

Mechi za wikendi hii zitakuwa za mwisho kabla ya dirisha la shughuli za usajili kuanza rasmi.

Usajili

AFC Leopards ni miongoni mwa timu zinazotarajiwa kusajili wachezaji kadhaa baada ya kocha, Casa Mbungo kusema anahitaji wachezaji sita kuimarisha kikosi chake.

Raia huyo wa Rwanda anaongoza kikosi ambacho kinakumbwa na majeruhi wengi, mbali na safu yake hafifu ya ushambuliaji inayojumuisha akina Marcel Kaheza, Wayi Yeka na Eugene Mukangula.

Ingwe ambao watacheza bila Isaac Oduro anayeuguza jeraha, watamtegemea nahodha Robinson Kamura kwenye safu ya ulinzi akisaidiana na Dennis Sikhayi, Isaac Kipyegon na Salim Abdalla wakati safu ya kiungo ikimilikiwa na Whyvonne Isuza.

“Ushindi wa majuzi ulitupa matumaini. Maishani lazima binadamu akumbane na changamoto, na sisi kama timu tumejiandaa kwa upinzani wowote,” Kamura alisema Ijumaa.

Kwa upande mwingine, Tusker wamekuwa wakipata matokeo yasiyoridhisha katika mechi zao za karibuni ambapo wameandikisha ushindi mmoja pekee katika mechi tano, lakini sasa wanatarajiwa kuwa makini zaidi katika mechi ya Jumamosi.

Walishindwa katika mechi yao ya kwanza mwezi huu waliponyukwa 1-0 na Nzoia Suagr ugenini katika mechi iliyochezewa Sudi, Bungoma.

Langoni, huenda kocha Robert Matano akamchezesha Emery Mvuyekure wakati safu ya ulinzi ikiwa mikononi mwa Marlon Tangauzi, Erick Ambunya, Hillary Wandera na Lloyd Wahome.