Presha Jubilee ilipe deni la Kalembe Ndile kabla ya mazishi yake

Presha Jubilee ilipe deni la Kalembe Ndile kabla ya mazishi yake

CHARLES WASONGA NA PIUS MAUNDU

CHAMA cha Jubilee kimetakiwa kilipe Sh6 milioni kwa familia ya marehemu Kalembe Ndile kwa mujibu wa makubaliano ya mwaka wa 2016 kabla ya mazishi yake Ijumaa wiki hii.

Suala hilo liliibuliwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Patrick Musimba aliyesema kuwa Jubilee iliahidi kumlipa mwanasiasa huyo pesa hizo kwa kukubali kuvunja chama chake cha The Independent Party (TIP) mnamo Novemba 2016.

Chama cha marehemu Ndile ni miongoni mwa vyama 13 vilivyovunjwa na kutoa nafasi ya kuundwa kwa Jubilee ili kuimarisha nafasi yake ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa 2017.

“Mheshimiwa Kalembe Ndile alifariki akidai Sh6 milioni alizoahidiwa na chama cha Jubilee kwa kukubali kuvunja chama chake cha TIP. Kwa hivyo, kwa heshima ya mwendazake naomba chama hiki kitoe pesa hizo kwa familia yake ili kugharimia mipango ya mazishi,” akasema Dkt Musimba.

Kauli yake iliungwa mkono na wabunge; Aden Duale (Garissa Mjini), Gitonga Murugara (Tharaka) na Makali Mulu (Kitui ya Kati) na kuibua mjadala mkali miongoni mwa wabunge.

“Jubilee ndicho chama chenye wabunge na maseneta wengi nchini na ndicho hopokea kiwango kikubwa cha fedha za hazina ya Vyama vya Kisiasa. Kwa hivyo, kiongozi wa wengi achukue hatua haraka ili kuhakikisha kuwa familia ya Ndile imelipwa kabla ya mwili wake kuzikwa. La sivyo chama hiki kishtakiwe,” akasema Bw Duale.

Lakini kiongozi wa wachache John Mbadi alionya kwamba deni hilo lisilipwe kutokana na mfuko wa pesa za umma.

“Sheria ya vyama vya kisiasa haina kipengele kinacholazimisha chama fulani kulipa deni la kisiasa. Kwa hivyo, pesa hizo zilipwe kutoka kwa mfuko wa wanasiasa binafsi,” akasema mbunge huyo wa Suba Kusini.

Mazishi

Wakati huo huo, baadhi ya wanasiasa wa chama cha Wiper na wakereketwa wengine ambao wamekuwa wakipanga kisiri mazishi ya Ndile walizozana na kamati inayoandaa mazishi hayo pamoja na familia ya mwanasiasa huyo.

Mgogoro huo wa wanasiasa unatishia kuyumbisha mipango ya mazishi ya mwanasiasa huyo yaliyopangwa kufanywa nyumbani kwake eneo la Mbui Nzau, kaunti ya Makueni Ijumaa wiki hii.

“Kalembe Ndile alikuwa mwanachama wa Wiper. Chama chapasa kudhibiti mipango ya mazishi haya,” alisema Bw Dee Kivuva, mkereketwa wa chama cha Wiper

Lakini mpango huo wa wakereketwa hao na wandani wa kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, ulimuudhi mjane wa Ndile, Magdalene pamoja na kamati ambayo imekuwa ikipanga mazishi hayo inayoongozwa na Mbunge mwakilishi wa kike Rose Museo pamoja na kiranja wa bunge la kaunti ya Machakos Mwengi Mutuse na Dkt Musimba.

Kamati hiyo ilisema Ndile alikuwa kipenzi cha kila mmoja.

You can share this post!

Naibu chifu afumaniwa akishiriki ngono na mwanafunzi

Wachezaji wa mitaa ya Nakuru wapokea ufadhili kupiga jeki...