Habari Mseto

Presha kwa mwanakandarasi kumaliza kujenga SGR hadi Naivasha

June 25th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Rais Uhuru Kenyatta amemtaka mwanakandarasi wa reli ya kisasa (SGR) kati ya Nairobi na Naivasha kutimiza ahadi ya kumaliza mradi huo kwa wakati unaofaa.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika Juni 2019. Akiongea Jumamosi Nairobi, Rais Kenyatta alisema analenga kutumia reli hiyo kuelekea Kajiado kwa sherehe za Madaraka mwaka ujao.

“Tunataka kutumia SGR kati ya Nairobi na Naivasha Mei 31 mwaka ujao kuelekea Kajiado kwa sherehe za kuadhimisha Madaraka,” alisema Rais Kenyatta.

Alisema hayo eneo la Kyang’ombe, Nairobi, alikoshuhudia kusakiniwa kwa madaraja juu ya Mbuga ya Wanyamapori ya Nairobi.

Ujenzi wa reli hiyo ya kilomita 120 ulianzishwa Oktoba 2016. Itapitia kaunti tano Nairobi, Kajiado, Kiambu, Nakuru na Narok.

Mwanakandarasi, Communications Construction Company (CCCC) alisema atamaliza mradi huo kwa wakati unaofaa kuambatana na mkataba.

Naibu Rais wa CCCC Chen Yun alisema wataongeza wafanyikazi kutoka Kaunti za Narok na Kajiado ili kumaliza mradi huo kufikia Juni 2019.