Habari Mseto

Presha kwa Shujaa katika michuano ya Hamilton Sevens

January 25th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA itakuwa na presha kubwa ya kufufua kampeni yake ya kusalia katika Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 itakapomenyana na Afrika Kusini, Scotland na Ufaransa katika mechi za Kundi C kwenye duru ya tatu itakayoandaliwa mjini Hamilton nchini New Zealand mnamo Januari 26, 2019.

Vijana wa kocha Paul Murunga wako nafasi moja kutoka mkiani katika ligi hii ya mataifa 15 baada ya kuzoa alama nne kutokana na duru mbili za ufunguzi zilizofanyika katika miji ya Dubai (Milki za Kiarabu) na Cape Town (Afrika Kusini) mwaka 2018.

Wako alama moja pekee mbele ya Japan. Timu inayoshikilia nafasi ya 15 baada ya duru zote 10 kusakatwa itapoteza nafasi yake katika Raga ya Dunia.

Kenya itakosa wachezaji wengi wazoefu wakiwemo Collins Injera, Billy Odhiambo, Eden Agero, William Ambaka na Andrew Amonde, ambao walisusia mazoezi kulalamikia mishahara kupunguzwa.

Inamaanisha kwamba tayari itaanza na unyonge fulani kwa sababu imesafiri na wachezaji wengi wapya ambao hawajacheza katika Raga ya Dunia ama msimu huu ndio wao wa kwanza.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kwamba Kenya imekuwa na ziara nzuri sana nchini New Zealand inapokutana na Scotland na Ufaransa.

Mara ya mwisho Kenya ilikutana na Scotland katika duru ya Hamilton ilishinda 33-19 katika robo-fainali ya kutafuta nambari tano mnamo Februari 4, 2018. Ilizabwa 19-15 na Samoa katika fainali na kuambulia alama 12.

Kabla ya hapo, Shujaa pia ilichapa Scotland 19-12 nchini New Zealand katika mechi za makundi mwaka 2015 na kuzimwa 19-5 na Afrika Kusini katika robo-fainali.

Kenya ilikutana na Ufaransa na Scotland katika makala ya mwaka 2014 ya duru ya New Zealand ikizishinda 24-7 na 24-14 katika nusu-fainali na fainali ya Bakuli, mtawalia.

Mwaka 2013, Kenya ilifanya vyema sana nchini New Zealand ikiwemo kuchapa Ufaransa 24-12 katika mechi za makundi, kushangaza Afrika Kusini 21-20 katika robo-fainali, kulemea wenyeji 19-14 katika nusu-fainali kabla ya kuzidiwa maarifa na Uingereza 24-19 katika fainali kuu.

Kenya ilibwaga Scotland 14-5 katika robo-fainali ya Bakuli mwaka 2012 nchini New Zealand. Ilikuwa imecharazwa 26-17 na Ufaransa katika mechi za makundi. Shujaa ililima Scotland 15-12 katika nusu-fainai ya Bakuli mwaka 2011.

Kenya ililemea Afrika Kusini 22-17 katika mechi za makundi nchini New Zealand mwaka 2009. Ilikutana na Afrika Kusini na Ufaransa katika mechi za makundi mwaka 2008. Ililemea Ufaransa 19-0, lakini ikapepetwa 33-7 na Afrika Kusini. Kenya ilibwagwa na Ufaransa 26-5 katika nusu-fainali ya Sahani mwaka 2007.

Chipukizi Daniel Taabu, Vincent Onyala na Johnstone Olindi waling’aa katika miji ya Dubai na Cape Town, licha ya kuwa Kenya haikufanya vyema. Macho yatakuwa kwao pamoja na nahodha mpya Jacob Ojee, ambaye anarejea katika Raga ya Dunia baada ya kukosa misimu mitatu iliopita.

Kundi A linaleta pamoja Fiji, Australia, Argentina na Wales nazo Marekani, Uingereza, Samoa na Tonga zinapatikana katika Kundi B. New Zealand, Uhispania, Canada na Japan zinakamilisha orodha ya washiriki 16 wa duru hii katika Kundi D.

Kikosi cha Kenya: Wachezaji – Daniel Taabu, William Reeve, Vincent Onyala, Brian Wahinya, Cyprian Kuto, Bush Mwale, Brian Wandera, Harold Anduvate, Michael Wanjala, Johnstone Olindi, Jacob Ojee (nahodha), Mark Wandetto Ruga na Eliakim Kichoi Mwasawa; Kocha – Paul Murunga.

Ratiba ya siku ya kwanza (Januari 26 kuanzia saa sita usiku na kuendelea):

Scotland na Ufaransa

Afrika Kusini na Kenya (00.22am)

Uingereza na Samoa

Marekani na Tonga

Australia na Argentina

Fiji na Wales

Uhispania na Canada

New Zealand na Japan

Scotland na Kenya (03.48am)

Afrika Kusini na Ufaransa

Uingereza na Tonga

Marekani na Samoa

Australia na Wales

Fiji na Argentina

Uhispania na Japan

New Zealand na Canada

Ufaransa na Kenya (08.00am)

Afrika Kusini na Scotland

Samoa na Tonga

Marekani na Uingereza

Argentina na Wales

Fiji na Australia

Canada na Japan

New Zealand na Uhispania