Presha kwa Solskjaer miti ya Man-Utd ikizidi kuteleza

Presha kwa Solskjaer miti ya Man-Utd ikizidi kuteleza

Na MASHIRIKA

KIUNGO Paul Pogba amesema Manchester United wana ulazima wa “kubadilisha mbinu zao za kutandaza soka” iwapo wana ndoto ya kusalia miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu.

Kichapo cha 4-2 ambacho Man-United walipokezwa na Leicester City waliotoka nyuma mnamo Jumamosi uwanjani King Power kiliwaondoa ndani ya mduara wa nne-bora jedwalini.

Mbali na kumzidishia kocha Ole Gunnar Solskjaer presha ya kupigwa kalamu, kichapo hicho pia kilikomesha rekodi ya kutopigwa kwa mabingwa hao mara 20 wa EPL katika mechi 29 zilizopita za ligi ugenini.

Mara ya mwisho kwa Man-United wanaohusishwa na kocha Zinedine Zidane kupoteza mechi ya ligi ugenini ni miezi 20 iliyopita.

Ilikuwa mara ya pili kwa chombo cha Man-United kuzamishwa kutokana na mechi tatu zilizopita za EPL na sasa wamejizolea alama moja pekee kutokana na tisa walizokuwa na uwezo wa kutia kapuni.

Man-United wamepoteza na kusajili sare ugani Old Trafford dhidi ya Aston Villa na Everton katika mechi mbili zilizopita ligini na walihitaji bao la sekunde za mwisho kutoka kwa Cristiano Ronaldo kupiga Villarreal 2-1 katika gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Septemba 29.

“Tumekuwa na mechi za aina hii kwa muda sasa. Iko shida kwa sababu tumefungwa na wapinzani kirahisi. Ipo haja kwa baadhi ya mambo kubadilishwa. Kuanzia kwa dhana ya wachezaji hadi kwa mbinu za ukufunzi,” akatanguliza Pogba katika mahojiano yake na Sky Sports.

“Iwapo maazimio ni kushinda ufalme wa EPL, hizi ni baadhi ya mechi ambazo tuna ulazima wa kushinda hata kama ni ngumu namna gani. Vinginevyo, mashabiki wataanza kututia presha na madhara yatakuwa makubwa,” akaongeza kiungo huyo wa zamani wa Juventus.

Kwa mujibu wa Phil McNulty ambaye ni mchanganuzi wa soka ya Uingereza, klabu ya Man-United kwa sasa imeisha makali kabisa chini ya Solskjaer na kila timu inachangamkia fursa ya kukutana nayo.

“Matokeo ya Man-United yanasikitisha na hawachezi kama timu iliyo na ari ya kushinda ligi. Sasa kila timu inataka fursa ya kucheza nao kwa sababu ni wanyonge,” akasema McNulty.

“Hali si shwari na hivyo ndivyo mambo yalivyo. Tulifungwa mabao ya haraka mwishoni mwa kipindi cha pili na hilo lilivuruga mpango wetu. Hofu ni kwamba pengo kati yetu na viongozi linazidi kuongezeka. Uthabiti wetu umeshuka na ratiba ijayo ni ngumu,” akasema Solskjaer ambaye hajashindia waajiri wake taji lolote tangu aaminiwe kuwa mrithi wa Jose Mourinho mnamo 2018.

Baada ya kumenyana na Atalanta ya Italia kwenye UEFA kesho kutwa ugani Old Trafford, masogora wa Solskjaer wataalika Liverpool ligini wikendi hii kabla ya kuvaana na Tottenham Hotspur, kurudiana na Atalanta na kuwaendea Manchester City katika EPL mnamo Novemba 6 ugani Etihad.

Man-United kwa sasa wana alama 14, tano nyuma ya viongozi wa jedwali Chelsea. Ni pengo la pointi tatu ndilo linatamalaki kati yao na mabingwa watetezi Man-City. Liverpool ambao hawajapoteza mechi yoyote kufikia sasa ligini msimu huu, wanakamata nafasi ya pili kwa alama 18.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):

Watford 0-5 Liverpool

Aston Villa 2-3 Wolves

Leicester 4-2 Man-United

Man-City 2-0 Burnley

Norwich 0-0 Brighton

Southampton 1-0 Leeds

Brentford 0-1 Chelsea

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kiunjuri aonekana kuasi Ruto na kujiunga na...

KDF yafichua ilivyoteka Kismayu na Al-Shabaab

T L