Michezo

Presha kwa Stars kuilima Equatorial Guinea wakikutana mara ya kwanza

May 28th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya wanaume ya Equatorial Guinea almaarufu Nzalang Nacional, italimana na wenyeji Harambee Stars uwanjani Kenyatta mjini Machakos, Mei 28, 2018.

Equatorial Guinea ilitua katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi hapo Mei 27 adhuhuri tayari kupimana nguvu na vijana wa kocha Sebastien Migne.

Mataifa haya mawili hayajawahi kukutana katika historia yao kwa hivyo mchuano huu unaweza kuenda upande wowote. Hata hivyo, Stars itaingia mechi hii na shinikizo kali baada ya kusikitisha dhidi ya Swaziland ilipolemewa 1-0 uwanjani Kenyatta mnamo Mei 25.

Kenya inarorodheshwa katika nafasi ya 111 katika viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) nazo Swaziland na Equatorial Guinea zinashikilia nafasi za 131 na 145, mtawalia.

Vijana wa Migne wataelekea mjini Mumbai kwa mashindano ya mwaliko ya Hero Intercontinental yatakayoleta pamoja India (wenyeji), Kenya, New Zealand na Chinese Taipei.

Stars inatumia michuano hii ya kirafiki kujiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019. Kenya inalimana na Ghana, Sierra Leone na Ethiopia katika mechi za Kundi F za kuingia AFCON.

Ilizimwa 2-1 na Sierra Leone katika mechi ya kwanza mwaka jana. Itaalika Black Stars ya Ghana mnamo Septemba 7, izuru Ethiopia (Oktoba 10), ialike Ethiopia (Oktoba 13) na kufunga mwaka huu dhidi ya Sierra Leone hapa nchini Novemba 16.