Michezo

PRESHA: Pochettino, Ole Gunnar katika shinikizo kuu

October 19th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MACHO yote yatakuwa kwa makocha Mauricio Pochettino (Tottenham Hotspur), Ole Gunnar Solskjaer (Manchester United) na Marco Silva (Everton) kuona mbinu watakazotumia kujinasua kutokana na presha kali inayowakabili wakati Ligi Kuu ya Uingereza itarejea leo Jumamosi.

Baada ya kumaliza Ligi Kuu ya msimu uliopita katika nafasi ya nne na pia kufika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya, Pochettino amejipata akiandamwa na shinikizo.

Hata gumzo limeibuka kuwa anakodolea macho kuangukiwa na shoka.

Hii ni baada ya vijana wake wa Spurs kuambulia ushindi mmoja katika mechi sita zilizopita katika mashindano yote ikiwemo kulipuliwa 7-2 na miamba wa Ujerumani Bayern Munich kwenye Klabu Bingwa na kuzidiwa ujanja kwa mabao 3-0 dhidi ya Brighton ligini katika mechi iliyopita.

Spurs inashikilia nafasi ya tisa ligini kwa alama 11 baada ya kusakata mechi nane. Itaalika Watford uwanjani Tottenham jioni katika mechi ambayo huenda ikamweka Pochettino pabaya zaidi akiipoteza.

Katika mechi hii, kocha wa Watford, Quique Sanchez Flores bado atakuwa akitafuta ushindi wake wa kwanza tangu achukue usukani baada ya Javi Gracia kupigwa teke mnamo Septemba 7 kwa msururu wa matokeo duni. Watford inavuta mkia kwa alama tatu na bila ushindi.

Pochettino atatumai mchuano huu utakuwa mwamko mpya kwa kikosi chake kinachojivunia wachezaji wakali kama Harry Kane, Lucas Moura, Moussa Sissoko na Son Heung-min.

Hata hivyo, Son pamoja na Christian Eriksen huenda wasijumuishwe kikosini kutokana na uchovu baada ya kusakatia timu zao za taifa za Korea Kusini na Denmark mtawalia mechi za kimataifa siku chache zilizopita. Kipa nambari moja Hugo Lloris yuko nje hadi mwezi Januari kutokana na jeraha la mkono. Paulo Gazzaniga anatarajiwa kudakia Spurs.

Nahodha wa timu ya Kenya, Victor Wanyama hajakuwa akitumiwa sana na kocha huyo kutoka Argentina na anatarajiwa kuwa shabiki wakati huu mashabiki wa Spurs hawataki kumuona uwanjani baada ya mchezo wake kushuka sana.

Spurs itaanza mchuano huu na takwimu nzuri za ana kwa ana za ushindi nane na sare tatu katika mechi 12 dhidi ya Watford kwenye Ligi Kuu.

Flores, ambaye amekuwa akiamini atasaidia Watford kukwepa kuteremshwa daraja, atakosa huduma za wachezaji kadhaa muhimu wakiwemo Etienne Capoue, Sebastian Prodl, Troy Deeney na Isaac Success. Wote wanauguza majeraha.

“Mashetani wekundu” wa United, ambao wako katika nafasi ya 12, wataalika viongozi Liverpool uwanjani Old Trafford katika mechi kubwa ya wikendi hii hapo kesho. Vijana wa Solskjaer wataingia katika mduara hatari wa kutemwa nambari 18 Everton ikilaza West Ham inayoshikilia nafasi ya nane. United kuingia katika mduara wa kutemwa hata hivyo, pia itategemea Aston Villa na Brighton kutoka sare nayo Newcastle ichape Chelsea pamoja na Southampton kuvuna alama tatu dhidi ya Wolves. Ripoti zimekuwa zikisema kuwa Solskjaer hatamaliza msimu huu uwanjani Old Trafford vijana wake wakiendelea kuzoa matokeo mabaya.

Kutoka orodha ya Pochettino, Solskjaer na Silva inaonekana Silva anakabiliwa na hatari zaidi ya kufurushwa. Vijana wake wamepoteza alama 12 baada ya kubwagwa na Bournemouth, Sheffield United, Manchester City na Burnley katika mechi nne zilizopita.

Inasemekana mechi dhidi ya West Ham ndiyo fursa ya mwisho ya Silva kujiokoa.

Ripoti zingine zinadai kuwa viongozi wa Everton wamempatia Silva mechi tatu kufufua timu la sivyo aachishwe kazi.

Mara ya mwisho West Ham ilizuru uwanjani Goodison Park ilivuna alama tatu baada ya kuchapa wenyeji wao 3-1 Septemba mwaka jana. West Ham ya kocha Manuel Pellegrini haina ushindi katika mechi tatu zilizopita katika mashindano yote.