Presha Raila amlipe Ruto deni la kisiasa

Presha Raila amlipe Ruto deni la kisiasa

TOM MATOKE Na ONYANGO K’ONYANGO

WASHIRIKA wa Naibu Rais William Ruto katika Rift Valley jana walimtumia Raila Odinga Jr kumtaka kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kulipa deni la kisiasa walilodai hajalipa tangu mwaka wa 2007.

Seneta wa Nandi Stephen Sang na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi walisema kwamba Bw Odinga alikuwa na deni la Dkt Ruto kwa kuchangia kufaulu kwake kwenye uchaguzi mkuu wa 2007. Katika uchaguzi huo, Bw Odinga alikuwa karibu kushinda urais.

Bw Odinga Jr alikuwa amemtembelea Bw Sudi nyumbani kwake Kapseret kabla ya wawili hao kuelekea Nandi Hills katika kaunti jirani ya Nandi kwa mazishi ya mchezaji maarufu wa gofu Gregory Koech, ambaye alikuwa rafiki yao wawili.

Katika hotuba yake, Bw Sudi alidai kwamba bila msaada wa Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2007, Bw Odinga angekuwa Waziri Mkuu, deni ambalo alisema limekomaa na linapaswa kulipwa 2022.

“Huwa ninamwambia Raila kwamba kwa sababu kuna kitu tunachotafuta, itakuwa bora tukianza mazungumzo sasa kwa sababu ana deni letu na suluhisho lake ni kulilipa. Mwaka kwa 2007, tulifunga barabara hadi Raila akiwa waziri mkuu kwa hivyo wakati mwingine mkiwa pamoja, mkumbushe kwamba Ruto ni mtu wetu,” Bw Sudi alimweleza Odinga Jr.

Kwa upande wake, Bw Odinga Jr, alikwepa suala la deni lakini akasema kama rafiki yake Gregory, urafiki unafaa kuvuka mipaka ya kikabila.

“Kama vijana, tunafaa kujifunza kwamba urafiki unavuka mipaka ya makabila kwa kuwa Kenya ni taifa kubwa. Hauwezi kuwa na marafiki kutoka kwa kabila lako pekee,” alisema.

Kitinda mimba wa Bw Odinga, alijiingiza katika mjadala kuhusu hasla na familia za watawala kati ya baba yake na Dkt Ruto, akisema kwamba watu hawafai kupimwa na wanakotoka kwa sababu wote hupambana kuwa na maisha mema.

“Hata kama umezaliwa mahali, haimaanishi kwamba wewe ni familia ya watawala,” alisema Odinga Jr.

Gavana Sang alisema kwamba ana matumaini kuwa Bw Odinga atalipa deni la kisiasa la Dkt Ruto ambaye ametangaza nia yake ya kugombea urais.

“Tunasubiri Raila alipe deni letu la kisiasa, Sudi amesema kwamba tunajenga daraja na Raila kwa sababu kufikia Disemba, siasa za Kenya zitabadilika,” alisema.

Gavana huyo aliongeza kuwa amani kati ya Wakalenjin na Waluo huvurugika kwa sababu ya siasa na kama viongozi, hawatakubali hilo kutendeka.

“Jamii za Wakalenjin na Waluo zimekuwa zikishirikiana katika biashara, kilimo na hazifai kuruhusu siasa kuzigawanya kwa kuwa siasa huja na kwenda na baadhi ya wanasiasa wanaotarajia zibaki maadui wataaibika,” alisema.

Bw Sang alifichua kuwa kutakuwa na mkutano kati ya viongozi wa jamii hizo mbili kutafuta suluhu ya alichosema kuwa “tofauti ndogo”.

Mwezi jana, Dkt Ruto, alipuuza uwezekano wake kuunda muungano na Bw Odinga kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.Alikanusha kwamba alikuwa ameanza mazungumzo na Bw Odinga akisisitiza kuwa siasa za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta zitakuwa mbio za farasi wawili.

Alisema hajawahi kuzungumza na Bw Odinga kuhusu suala la kuungana akisisitiza kuwa waziri mkuu huyo wa zamani ni mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi mkuu ujao.na, akiwa Ngeria Technical Training Institute (TTI) katika eneobunge lake, Bw Sudi alidai kwamba wamekuwa wakizungumza na Bw Odinga awasaidie kuhakikisha kuwa Jubilee itaheshimu sheria.

“Ninapomuona Raila Odinga, huwa ninamuona mpinzani wake 2022, kwa hakika, kwangu, Raila ndiye ninayeweza kushindana naye 2022 na sijui siasa za Kenya zitakuwaje ikiwa Raila Odinga atakuwa mpinzani wake, nani atakuwa mpinzani wangu basi?” alihoji.

You can share this post!

NMG yatenga siku ya matumizi ya Kiswahili mara moja kila...

Mwanamke atoroka mumewe na kuolewa na ‘roho mtakatifu’