Michezo

Presha ya kunoa Man-United imenizeesha haraka – Ole Gunnar Solskjaer

December 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer amesema ana matumaini kuwa kikosi chake cha Manchester United kitaiamarika zaidi na kurejea kuwa miongoni mwa wagombezi halisi wa mataji ya soka ya Uingereza na barani Ulaya.

Akiadhimisha miaka miwili ya ukufunzi kambini mwa Man-United waliowahi pia kujivunia huduma zake akiwa mchezaji, Solskjaer, 47, alisema mvi zake zinaongezeka kila uchao kwa sababu ya presha ya kazi anayoifanya uwanjani Old Trafford.

“Tulitinga nusu-fainali za mapambano matatu muhimu mnamo 2019-20 na tukaingia ndani ya mduara wa nne-bora kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Hizo ni ishara ya kuimarika na kuboreka kwa kikosi,” akatanguliza Solskjaer.

Kwa mujibu wa kocha huyo raia wa Norway, ushindi katika mchuano wa ziada walio nao utawapa motisha zaidi katika kampeni za msimu huu kwa kuwa watakuwa wameanza kujongea kileleni mwa jedwali la EPL.

“Ingawa tumeondolewa tayari kwenye kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), muhimu zaidi ni kuangalia mbele na kutazamia yajayo,” akaongeza.

“Nimefurahia kuwa kocha wa Red Devils kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita. Hata hivyo, zipo baadhi ya mechi ngumu kama ile ya majuzi iliyotukutanisha na Sheffield United. Hiyo ni mifano ya michuano ambayo inazidi kunipa presha na kuniongezea mvi. Nyakati za mechi sampuli hiyo, kocha na mashabaki huhitajika kuwa na mioyo ya vyuma,” akasisitiza.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Leeds United ambao watakutana nao kwa mara ya kwanza baada ya takriban miaka 17 mnamo Disemba 20, 2020.