Michezo

Presha ya mashabiki kwa Ingwe irarue Wazito FC

August 29th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

MASHABIKI wa AFC Leopards wametaka timu yao imalizie hasira yake kwa Wazito FC zitakapokutana katika mechi ya Ligi Kuu ya raundi ya 29 uwanjani Kenyatta mjini Machakos, Jumatano.

Leopards ilipepetwa na timu ya pili ya Gor Mahia kwa mabao 2-0 katika gozi la ‘Mashemeji’ uwanjani Kasarani katika mechi yake iliyopita na mashabiki sasa wameitaka iwaondolee aibu kwa kupata ushindi dhidi ya Wazito inayokodolea macho kutemwa baada ya msimu mmoja kwenye Ligi Kuu.

Shabiki Nick Otwande amesema, “Naenda kushabikia timu yangu ya Ingwe. Hasira itaishia hapa.”

Mashabiki wengi wa Leopards wameonya timu yao dhidi ya kuteleza leo. Raps Vander Villa, “Msituaibishe…” Albert Kachero Oungo, “Natumaini hamtatusikitisha dhidi ya Wazito kwa sababu hata siamini kwamba timu ya pili ya Gor Mahia ilitulima.”

Zilipokutana kwa mara ya kwanza kabisa ligini, Ingwe ilitolewa jasho na Wazito kabla ya kuishinda 3-2 mnamo Machi 14, 2018. Pistone Mutamba, ambaye sasa ni mali ya Sofapaka, alifungia Wazito mabao yote. Whyvonne Isuza alipachika mabao mawili ya mwisho ya Leopards naye Ezekiel Odera akapata bao moja.

Odera, ambaye anaongoza katika kufungia Ingwe mabao baada ya kuona lango mara 11, hatashiriki mchuano huu. Anatumikia marufuku ya mechi mbili baada ya kufikisha kadi tano za njano na moja nyekundu. Alikosa mechi ya Gor na atakamilisha marufuku yake dhidi ya Wazito.

Ratiba (Agosti 29, 2018):

Kariobangi Sharks na Thika United (2.00pm, Machakos), Posta Rangers na Sofapaka (2.00pm, Camp Toyoyo), Tusker na Chemelil Sugar (3.00pm, Ruaraka), Ulinzi Stars na Nakumatt (3.00pm, Nakuru), Wazito na AFC Leopards (4.15pm, Machakos).