Habari

Presha yapanda kambi ya Ruto

July 5th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WANASIASA wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto wanakabiliwa na presha kali kutoka kwa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta za kuwataka wasaliti uaminifu wao kwake.

Tayari wabunge kadhaa hasa kutoka Mlima Kenya, Pwani na Kisii wamesalimu amri baada ya kuzidiwa na joto la siasa kwa kutoroka kambi ya Dkt Ruto.

Mbinu ya kwanza ilikuwa ni kuwapokonywa nyadhifa washirika wa Dkt Ruto katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Kwa sasa baadhi ya wale ambao wamekataa kupiga magoti wameanza kuandamwa nje ya bunge kwa madai ya ufisadi dhidi yao na pia polisi kutumika kuvuruga mikakati ya wengine.

Baadhi nao wametumiwa jumbe za kuwashawishi kubadili misimamo kwa ahadi za kupewa vyeo serikalini.

“Kuna juhudi za kuwahangaisha wandani wa Dkt Ruto kwa kila mbinu, japo kuna wale ambao bado wamekwama kwake. Kuna uwezekano mkubwa kuwa ni wale wa kutoka ngome yake ya Rift Valley watakaobaki naye hadi 2022. Baadhi ya wanaotoka maeneo mengine wanaweza kuingizwa baridi kabla ya wakati huo,” asema mdadisi wa siasa Paul Katana.

Kati ya wale ambao wamekimbia kambi ya Dkt Ruto ni Catherine Waruguru (Mwakilishi wa Wanawake Laikipia) na wabunge Sarah Kolele (Laikipia Kaskazini), Ali Wario (Garsen), Paul Katana (Kaloleni), Gichimu Githinji (Gichugu), John Wambugu (Kirinyaga ya Kati) na Kabinga Wachira (Mwea).

Wengine waliohepa ni Ezekiel Machogu (Nyaribari Masaba), John Oyioka (Bonchari) na Richard Onyonka (Kitutu Chache).

Lakini kuna wale ambao bado wamesimama ngangari kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Katika eneo la Magharibi ambalo Rais Kenyatta ameanza juhudi za kuzima upenyo wa Dkt Ruto, baadhi ya waliosisitiza kusimama nyuma yake ni aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale na wabunge Didimus Baraza na Benjamin Washiali ambaye alipokonywa wadhifa wa kiranja wa wengi bungeni.

Mwishoni mwa Juni 2020 Bw Washiali aliongoza wabunge wanaomuunga mkono Dkt Ruto kufanya mkutano nyumbani kwa Mbunge wa Malava, Malulu Injendi ambao ulivurugwa na polisi.

Licha ya kupokonywa nyadhifa katika Seneti, maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Kithure Kindiki (Tharaka Nithi), Susan Kihika (Nakuru) na Mithika Linturi (Meru) bado wamekwama kambi ya Ruto.

Pia kuna Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot na mwenzake wa Nandi Samson Cherargei pamoja na Gavana Stephen Sang.

Wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Caleb Kositany (Soy) na Kimani Ngunjiri (Bahati) nao wamekuwa mstari wa mbele kutangaza uaminifu wao kwa Dkt Ruto.

Katika eneo la Mlima Kenya wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), Rigathi Gachagua (Mathira), Ndindi Nyoro (Kiharu), Alice Wahome (Kandara) na Kimani Ichung’wa (Kikuyu) wamenata kwa Dkt Ruto licha ya presha kali kuwakumba.

Bw Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, tayari wanachunguzwa kwa madai ya ufisadi.

Katika eneo la Ukambani, Dkt Ruto amesajili aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama kuungana na wabunge Victor Munyaka na Vincent Musyoka kumpigia debe.

“Kwa sasa nafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Ruto atakuwa Rais wa tano wa Kenya mwaka wa 2022. Mimi sio mtu wa kutishwa na siogopi kwa sababu nina haki ya kuamua mwelekeo wa kisiasa ninaotaka,” Bw Muthama aliambia Taifa Jumapili.

Katika eneo la Pwani, Naibu Rais amebaki na wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Mohammed Ali (Nyali) na Khatib Mwashetani (Lunga Lunga).

Aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar pia amejiunga na kikosi cha Dkt Ruto.

Kaskazini Mashariki anaungwa mkono na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale ambaye alipokonywa wadhifa wa kiongozi wa wengi bungeni na Mbunge wa Wajir Mashariki, Ahmed Kolosh.