Makala

Presha za Joe Nyutu Murang’a iimarike

March 31st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

PRESHA za Seneta Joe Nyutu wa Murang’a kwa serikali ya kitaifa na kaunti zimeishia kuzaa matunda kemkem ya kimaendeleo kwa manufaa ya wenyeji.

Huku maseneta wakiwa bila hazina ya kutekeleza maendeleo mashinani, mdomo umegeuka kuwa kifaa chao kusaka maendeleo.

Ni mbinu ambayo Bw Nyutu amekuwa akitumia kwa weledi na katika hali zingine, kumwacha akipambana na athari za kupigwa kisiasa na waliosinywa.

Mwaka wa 2023 Nyutu alizindua harakati kuteta Murang’a ilikuwa ikipokezwa mgao wa hazina kuu usioambatana na vigezo husika na ndipo katika ratiba iliyotangazwa, kaunti ikaongezwa Sh1 bilioni.

“Tulikuwa tukipokezwa Sh5 bilioni katika utawala wetu wa Gavana wa kwanza Bw Mwangi wa Iria. Kwa sasa tunapata Sh6 bilioni baada ya mimi kupiga kelele katika bunge la kaunti,” asema.

Bw Nyutu aidha aliteta kuhusu ukosefu wa shamba la kujenga kiwanda cha uongezaji ubora mazao ya wakulima, hali ambayo iliishia serikali ya Kaunti ya Murang’a kutenga ekari 1,400 kutoka shamba la kampuni ya Del Monte ili kufanikisha mradi huo.

Bw Nyutu alitifua kivumbi kuhusu suala hilo hadi Rais William Ruto akiwa katika ziara ya kikazi kaunti hiyo akashangaa naye.

“Huyu Seneta Nyutu ametoa kizungu kingi hadi shamba la Del Monte likapatikana,” akasema.

Bw Nyutu aidha aliteta kuhusu suala la ukiukaji wa haki za kibinadamu miongoni mwa masoja wa Del Monte ambao walikuwa wakituhumiwa kuua, kushambulia na kulemaza na pia kubaka wanawake katika shamba hilo la mananasi la ekari 28, 000.

“Kufikia sasa, kampuni hiyo imefunguliwa mashtaka katika mahakama kuu ya Thika kuhusu ukiukaji wa haki za majirani wake huku baadhi ya wateja wa kimataifa wa bidhaa za Del Monte wakizisusia kwa msingi wa visa hivyo,” Bw Nyutu akasema.

Aliongeza kwamba kufikia sasa kampuni hiyo imefuta walinzi wake 250 kwa msingi wa kutafuta njia ya kujitakasa kuhusu haki za wenyeji na kuajiri wapya kutoka kwa kampuni ya G4S.

Mwaka jana, 2023 Bw Nyutu aliteta kwamba huduma za hospitali katika Kaunti ya Murang’a zilikuwa zimezorota na pia kiwanda cha kaunti cha wakulima wa maziwa kilikuwa kimesambaratika hadi kufungwa.

“Kufikia sasa huduma za hospitali zimeimarishwa si haba baada ya mimi kupeleka kamati ya Seneti hadi kwa hospitali kadha za kaunti kutathmini hali. Kisha nikawapeleka maseneta wa kamati ya viwanda hadi Murang’a na kwa sasa kiwanda hicho cha maziwa kimefunguliwa upya,” akasema.

Tetesi kali za Bw Nyutu zilizuka Februari ambapo aliteta kwamba Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alikuwa amegeuka kuwa mdhalimu na mjeuri.

Bw Nyutu alipendekeza Bw Gachagua afutwe kazi na badala yake wadhifa huo ukabidhiwe Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro.

Katika siasa zilizozuka, Rais William Ruto alizindua ziara katika kaunti hiyo ambazo zililenga kutuliza hali tete iliyokuwa ikisambaa kutokana na matamshi ya Bw Nyutu.

Rais alizindua miradi ya barabara, maji, mahospitali na pia ya stima.

Bw Gachagua naye alizindua ziara kadha za kujitafutia udhibiti na ambapo hadi sasa amefika Murang’a mara nne akitoa ahadi za maendeleo na pia kutoa Sh1 miliona za kupiga sherehe katika chuo kikuu cha Murang’a kilichoko katika ngome ya Bw Nyoro.

Bw Nyutu anasema kwamba atazidi kutumia mdomo wake ili kupeleka maendeleo Murang’a.

[email protected]