Michezo

Prisons yampa Agala utepe tayari kwa CAVB

February 28th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BRACKCIDES Agala amepokezwa utepe wa unahodha wa kikosi cha Kenya Prisons kitakachowania ufalme wa Klabu Bingwa barani Afrika (CAVB) kwa voliboli ya wanawake Machi 2019 jijini Cairo, Misri.

Agala alikosa makala yaliyopita kutokana na majukumu ya uzazi.

Anatwaa unahodha kutoka kwa mvamizi Evelyne Makuto aliyewaongoza Prisons kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya Voliboli (KVF) mwishoni mwa msimu jana.

Brackcides Agala (kulia) na Evelyne Makuto wakiichezea Kenya Pipeline . Picha/ Maktaba

Prisons ambao waliambulia nafasi ya nne katika fainali za voliboli ya kimataifa zilizoandaliwa mwaka jana nchini Misri, walianza kujinoa hapo jana mjini Ruiru.

Akitetea uteuzi wa Agala, kocha Josp Barasa wa Prisons alisema kipusa huyo ni miongoni mwa wanavoliboli wanaojivunia tajriba pana katika ulingo wa mchezo huo.

“Mbali na ustadi wake, ana uzoefu wa kina katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa hasa ikizingatiwa kwamba amekuwa tegemeo kubwa katika kikosi cha kitaifa,” akatanguliza.

“Amekuwepo kwa muda huu wote na yupo katika nafasi bora zaidi ya kuongoza kikosi kitakachotamalaki mapambano ya kimataifa muhula huu nchini Misri kati ya Machi 16-15,” akaongeza Barasa na kusisitiza kwamba Agala ni mchezaji na kiongozi ambaye ni kielelezo kwa wanavoliboli wengi katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Chini ya Makuto, Prisons walitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya msimu jana kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka mitano.

“Makuto alidhihirisha uongozi bora kikosini. Ni wakati wake ambapo tulikomesha ukame wa mataji ya voliboli ligini. Nina wingi wa imani kwa Agala na chini yake, tutakuwa na kila sababu ya kujizolea mataji mengi zaidi hasa katika ulingo wa kimataifa,” akasema kocha Barasa.

Mbali na hamasa tele inayotawala kikosi chake, Barasa amefichua kwamba kikosi chake hakina visa vyovyote vya majeraha.

“Idara zote za kikosi ziko imara. Muhimu kwa sasa ni kujipa msasa na kujiimarisha zaidi. Viwango vya ushindani miongoni mwa wachezaji vinaridhisha na ninaamini Prisons ni wagombezi halisi wa taji mwaka huu,” akaongeza Barasa ambaye pia ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya voliboli, Malkia Strikers.

KIKOSI: Herman Jepyegon, Joy Lusenaka, Mercy Likhayo, Edith Wisa, Shyren Jepkemboi, Diana Khisa, Lauren Chebet, Brackcides Agala, Immaculate Chemutai, Lydia Maiyo, Yvonne Wavinya, Meldine Sande, Evelyne Makuto, Loice Tarus, Joan Chelagat, Judith Trus, Elizabeth Wanyama, Pamela Masaisai, Teresa Ewet na Caren Cheruto.