Michezo

Prisons yapaa, Pipeline yajikwaa Nanyuki

September 15th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WANAUME wa Kenya Prisons walisajili pointi tisa muhimu kwenye mechi za voliboli ya Ligi Kuu ya KVF zilizochezewa mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia Ijumaa.

Nao malkia wa zamani, Kenya Pipeline ya kocha, Margaret Indakala ilidondosha alama moja muhimu baada ya kutolewa kijasho kikali kabla ya kushinda 3-2 dhidi ya mabingwa watetezi, Kenya Prisons.

Kwenye mchezo huo Pipeline na Prisons zilikosa huduma za kati ya maseta mahiri nchini, Janet Wanja na Jane Wacu mtawalia ambao wamo nchini Japan kushiriki voliboli ya Kombe la Dunia.

Licha ya kuyeyusha pointi moja muhimu, Pipeline ilinasa ufanisi huo kwa alama 25-19, 25-27, 25-16, 24-26, 19-17.

Naye Ernestine Akimanizanye sajili mpya kutoka Rwanda aliisaidia KCB kuvuna ushindi wa seti 3-0(25-17, 25-14, 25-10) mbele ya Ulinzi (KDF).

Nao madume wa Kenya Prisons waliandikisha ushindi wa mechi mbele ya Administration Police of Kenya (AP Kenya), Kenya Army na Ulinzi (KDF).

Kikosi hicho chini ya kocha, Paul Muthinja kilishinda AP Kenya seti 3-1 (34-36, 25-21, 25-18, 25-14), Kenya Army seti 3-0 (25-23, 25-17, 25-19) na KDF seti 3-1 (25-20, 19-25, 25-15, 25-21).

Nao mabingwa watetezi, Kenya General Service Unit (GSU) ilijiongezea alama tatu muhimu ilipochoma KDF kwa seti 3-0 (25-18, 25-16, 25-23). Baada ya KDF kupoteza mechi mbili ilifanikiwa kujifariji ilipokung’uta Equity Bank kwa seti 3-0 (25-19, 28-26, 25-19).

Kwenye matokeo mengine ya wanaume, Kenya Army ililimwa seti 3-1 na Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA), Nairobi Prisons ilipoteza mechi kwa seti 3-0 kila moja mbele ya Equity Bank na KPA nayo AP Kenya iliichapa Kenya Army seti 3-0.