Michezo

Pro Soccer yaitoa Kinyago United kijasho

September 30th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Pro Soccer Academy ilishindwa kiume ilipoteleza na kuchapwa bao 1-0 na Kinyago United kwenye mechi ya Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 iliyopigiwa uwanjani KYSD Kamukunji, Nairobi.

Nayo MASA iliidhalilisha Fearless Academy kwa magoli 10-1 huku Young Elephant ikitwaa pointi tatu bila jasho ikiwa ni ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao Volcano FC kuingia mitini.

Kinyago United ambayo ndiyo mabingwa watetezi ilipata mtihani mgumu mbele ya wapinzani wao kabla ya kubahatika kunasa goli la pekee lililofunikwa kimiani na Jahson Wakachala.

”Dah! Kusema kweli soka haina heshima tulipata ushindi wetu kwa neema yake Mungu hatuna budi kumshukuru. Wapinzani wetu waliteremsha mchezo wao kivingine hali iliyotufanya kupoteza mwelekeo lakini nao walikosa ujanja kabisa hawakubahatika kupenya katika ngome yetu,” nahodha wa Kinyago, Samuel Ndonye alisema.

MASA ilipata mteremko mbele ya wapinzani wao na kujiongezea alama tatu muhimu. Wafungaji wa MASA walikuwa: Gabriel Otieno, Eshele Konivya, Levy Momanyi na Randy Omondi kila mmoja alicheka na wavu mara mbili, nao Brandy Jeroi na Nowel Owino waliitingia bao moja kila mmoja. Telen Ochieng aliifungia Fearless Academy goli la kufuta machozi.

Hata hivyo MASA iliendelea kukamata tano bora kwa alama 22, baada ya Sharp Boys kurukia tatu bora ilipodunga Locomotive FC mabao 3-1.

Victor Aguya alitikisa wavu mara mbili naye Michael Okutoyi aliitingia goli moja. Nayo Locomotive ilijipatia bao la kufuta machozi kupitia David Mwangi.

Katika msimamo wa ngarambe hiyo, Kinyago United inazidi kukaa kileleni kwa kufikisha alama 36 baada ya kushinda mechi zote 12.

Fearless FC iliangusha Pumwani Ajax kwa mabao 3-1 na kuendelea kufunga mbili bora kwa alama 28, nne mbele ya Sharp Boys.

Kwenye matokeo hayo, Young Achievers ilijipata njiapanda ilipozimwa mabao 2-0 na Lehmans, Pumwani Foundation iliikandamiza State Rangers kwa magoli 4-0 nayo Gravo Legends ilitoka sare tasa na Tico Raiders.