Michezo

Pro Soccer yalenga kubeba taji la KYSD

August 19th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Pro Soccer Academy ni miongoni mwa vikosi ambavyo vimezamia mpango mzima wa kukuza talanta za wanasoka wanaoibukia mtaani Kaloleni na jiji la Nairobi kwa jumla.

Waanzilishi wa timu nyingi hapa nchini wamekuwa mstari wa mbele kutumia fani mbali mbali ikiwamo soka kuwaleta vijana pamoja ili kuwaepusha dhidi ya matendo maovu mitaani.

”Kusema kweli bila kuzipigia debe shughuli tunazotekeleza soka ya hapa nchini imesaidia chipukizi wengi, wavulana na wasichana hasa kutambua talanta zao wakiwa wadogo,” anasema kocha wake, Davis Shem Odongo na kuongeza kuwa hatua ya kubuniwa kwa timu za soka imechangia visa vya uhalifu katika Kaunti ya Nairobi kupungua kwa asilimia kubwa.

Kocha huyo alianza kunoa chipukizi wa kikosi hicho mwaka 2015 baada ya mwanzilishi wake, Zablon Otieno kufariki.

”Nina imani tosha kuwa tukifaulu kupata ufadhili tu tutafanya makubwa katika harakati za kunoa makucha ya wanasoka chipukizi. Ukosefu wa udhamini huchangia timu nyingi kuvunjiliwa mbali hata hivyo ninashukuru wazazi wa chipukizi wa kikosi changu bila kusahau mwakilishi wa Wadi ya Kaloleni, Nicodemus Ochieng kwa kutuunga mkono,” alisema. Kwa jumla Pro Soccer Academy ina timu kadhaa za vitengo tofauti kulingana na umri ambazo ni: (U7, U9, U11, U13 na U15).

”Kikosi changu cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 14 ndio mwanzo kinashiriki Ligi ya KYSD lakini nina imani tukijitahidi kwenye mechi zetu tumekaa vizuri kuwapiku washiriki wengine na kubeba taji la msimu huu,” alisema na kuongeza kuwa hana hofu na kikosi chake.

Kocha huyo anajipiga kifua na kutaja kuwa Kinyago United pekee ndio tisho kwa chipukizi wake maana itakuwa katika ardhi ya nyumbani tena mbele ya wafuasi wao. Anadai kuwa chipukizi wake wamejaa motisha baada ya kucheza mechi tano, kushinda tatu, kutoka nguvu sawa mchezo mmoja kisha kudondosha patashika moja kwenye kampeni za kipute cha msimu huu.

Anatoa mwito kwa wahisani wajitokeze na kuzipiga jeki timu za wachezaji chipukizi mashinani kwenye juhudi za kupalilia talanta zao ili kuibuka wa kutajika miaka ijayo.

Pro Soccer Academy ya wasiozidi umri wa miaka 14 ina wachezaji kama: Dibone Otieno, Jamaine Otieno, Thomas Okila, Nick Ochieng, Stallone Odhiambo, Boniface Mwangi, Robert Omondi, Anthony Oduor, Rashid Juma, Daniel Amboka, Amos Shabban na Sheldon Kabiki. Kinyago United ya kocha, Anthony Maina ndio mabingwa watetezi huku ikijivunia kushinda taji hilo mara 12 tagu ligi hiyo ianzishwe mwaka 2000.