Habari Mseto

Prof Ghai ataka fedha zilizotumika na Jubilee Ikulu ziwekwe wazi

May 8th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

SHIRIKA moja lisilo la kiserikali, limeandikia barua Msimamizi wa Ikulu Bw Kinuthia Mbugua, likitaka aeleze kiwango cha pesa zilizotumiwa kuandaa mikutano ya chama cha Jubilee katika Ikulu ya Nairobi na ikulu ndogo nchini mwaka 2017.

Katiba Institute, linataka kujua gharama ya mikutano yote ambayo chama cha Jubilee kiliandaa katika ikulu wakati wa kampeni, aliyeitisha mikutano hiyo na aliyesimamia gharama.

“Dhamira ya barua hii ni kuomba habari kuhusu gharama iliyotokana na mikutano ya chama cha Jubilee katika Ikulu na Ikulu ndogo kati ya Septemba 2, 2017 na Oktoba 2, 2017,” inasema barua iliyotiwa sahihi na mwenyekiti wa shirika hilo Prof Yash Pal Ghai.

Shirika hilo linataka Bw Mbugua kueleza ikiwa Ikulu ni ukumbi wa kukodishwa kuandaa mikutano na ada inayotozwa.

“Je, Ikulu inaweza kukodishwa kuandaa mikutano ya vyama vya kisiasa au hafla zinazoegemea upande mmoja, na ikiwa inakodishwa, ada ni gani?” aliuliza Prof Ghai.

Anataka Bw Mbugua au afisa anayehusika, kueleza aliyelipa gharama ya kukodisha ikulu, vinywaji na mlo katika kila mkutano.

“Unaweza kutukabidhi nakala za risiti, hati za kutoa huduma zilizotolewa kwa kila mkutano,” anaomba kwenye barua aliyoandika Mei 4 mwaka huu.

Profesa Ghai anataka maafisa wa ikulu kueleza iwapo gharama ililipwa na wahusika wengine kikiwemo chama cha Jubilee, pesa walizolipa na risiti za kuthibitisha kwamba walilipa pesa hizo.

“Ikiwa serikali ililipa gharama ya kuandaa mikutano hiyo, ni maafisa gani walioidhinisha malipo hayo. Ikiwa serikali ililipa gharama ya kuandaa mikutano hiyo ilitumia pesa ngapi,” mtaalamu huyo wa katiba anataka kujua.

Aidha, anataka maafisa hao waeleze iwapo pesa za kuandaa mikutano hiyo zilikuwa zimetengwa kwenye bajeti na jina la kila afisa aliyeidhinisha pesa hizo kutumika.

Profesa Ghai anaambatisha orodha ya mikutano 12 ambayo wajumbe wa chama cha Jubilee wakiwemo wabunge walitembelea ikulu kukutana na rais kabla ya marudio ya kura ya urais ya Oktoba 26 mwaka jana.

“Iliripotiwa katika vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na tovuti rasmi ya ofisi ya rais kwamba Rais aliandaa mikutano kadhaa katika ikulu na ikulu ndogo kuhusu masuala ya chama cha Jubilee na kwa kampeni zake pamoja na mikutano ya kundi la wabunge la chama cha Jubilee,” anasema Prof Ghai.

Kulingana naye, Rais alipokea wajumbe wa chama cha Jubilee kutoka maeneo kadhaa kote nchini katika ikulu walioahidi kumuunga mkono.

Anasema anatoa ombi hilo chini ya sheria ya haki ya raia kupata habari kutoka kwa serikali, na haki ya serikali kuchapisha habari kwa manufaa ya wananchi na iwapo haitampa habari hizo ataishtaki mahakamani.