Lugha, Fasihi na Elimu

Prof Katana awataka walimu kutowatwika wazazi lawama zote za moto shuleni

February 13th, 2024 2 min read

NA MAUREEN ONGALA

ALIYEKUWA mwenyekiti wa Bodi ya Elimu ya Kaunti ya Kilifi Gabriel Katana amewataka wasimamizi wa shule za upili kutowalimbikizia lawama wanafunzi wakati shule zinapochomeka na badala yake kufanya uchunguzi wa kina. 

Kulingana mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pwani, visa vya uchomaji wa shule kwa sasa vimechukua mkondo mpya, swala ambalo linastahili kuzingatiwa kwa uzito.

Akizungumza na wanahabari mjini Kilifi, Prof Katana alisema kuwa walimu wakuu na wanachama wa bodi za shule wamekuwa na haraka sana kuwanyooshea kidole wanafunzi shule zinapochomwa.

“Huko nyuma tumekuwa na visa kama hivyo na tunapoangalia kwa kina tunaona kuna msukumo wa watu ambao sio wanafunzi,” akasema Prof Katana.

Alitoa mfano wa shule ya upili ya Dr Krapft Memorial ambayo ilipata upinzani mkubwa kutoka kwa mabwanyenye wakati ilibadilishwa kutoka kwa shule isiyo ya malazi na kuwa shule ya bweni.

Bweni la Mississippi likiteketea shuleni Mariakani. PICHA | ALEX KALAMA

Prof Katana alisema wakati shule hiyo haikuwa ya malazi, mabwanyenye wengi walikuwa wamejenga nyumba za kuishi ambazo waliwakodishia wanafunzi.

“Nyumba hizo zilikuwa zinawapa matajiri hao pesa nyingi kupitia kwa kodi na ilipotangazwa kuwa shule hiyo itakuwa shule ya bweni, walikasirika na kuwachochea wanafunzi kuchoma mabweni,” akadai.

Alisema wakati huo, yule mwanafunzi aliyeongoza uchomaji wa mabweni katika shule ya Dr Krapf Memorial alienda na kuwashawishi wasichana wa shule ya upili ya Mazeras kuchoma shule. Wao hawakuwa na sababu kama zao.

“Hata walimu wanakosa kuwa na nia nzuri na maendeleo ya wanafunzi na huwachochea kuchoma shule,” akaongeza kuibua madai.

Ilibainika ya kwamba matroni wa shule ya wasichana ya St John katika eneobunge la Kaloleni Bi Irene Kerubo Mauti ndiye aliyechoma bweni mnamo Januari 31, 2024.

Bi Mauti alinaswa kwa camera za CCTV akiingia katika bweni hilo na moto ukalipuka baada ya dakika mbili alipotoka.

Prof Katana alisema kuwa pia wakati wa kuchoma shule umebadilika ghafla kwani ilikuwa kawaida kuwa wanafunzi waligoma na kuchoma shule muhula wa pili kwa kile kilichodaiwa kuwa walikuwa wanaogopa kufanya mitihani, lakini mtindo huo umebadilika na kushuhudiwa katika muhula wa kwanza.

“Hapo nyuma uchomaji wa shule ulikuwa ukiangaziwa katika muhula wa pili kwa sababu kulikuwa na mitihani na ikasemekana kuwa watoto wetu wanaogopa mitihani na eti walifanya hivyo wakitaka sababu ya kuenda nyumbani,” akasema.

Kwa sababu hiyo, alisema kuna umuhimu wa kutaka kujua ni kipi kilichobadilika katika shule nyingi ambacho kinasababisha uchomaji wa shule katika muhula wa kwanza.

“Hili ni swala linalosumbua akili. Ni sharti tulizingatie na kujiuliza kwa nini katika shule zetu mambo yamebadilika na tuone jinsi ya kurekebisha hali,” akasema.

Hata hivyo, Prof Katana alieleza kuwa hali ya kutojali umuhimu wa elimu ya mtoto wa Kilifi miongini mwa viongozi wakuu wa elimu katika kaunti hiyo imechangia pakubwa katika changamoto nyingi zinazoendelea kushuhudiwa katika sekta ya elimu.

Alisema wasimamizi hao wamekosa kutekeleza mapendekezo mbalimbali ya kukomboa sekta ya elimu.

Alieleza kuwa alipokuwa mwenyekiti wa bodi, walizingatia namna ya kuzima migomo ya wanafunzi na uchomaji wa shule na kuweka mikakati ya kuboresha mafanikio ya wanafunzi katika mitihani ya kitaifa.

Walibuni kamati ambazo zilihusisha shule za kitaifa katika kaunti ya Kilifi na zile za kaunti.

“Tulianza msusururu wa kuwaita walimu walezi wa kila shule na wale wanaohusika na maswala ya akademia ili kuwasaidia walimu kupata matokeo bora,” akasema.

Alisema inasikitisha kuwa mtoto wa Kilifi ambaye atajiunga na shule ya upili nje ya kaunti hiyo atafanya vizuri katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) lakini atafanya vibaya anapoijiunga na shule zilizoko Kilifi licha ya kufanya vizuri katika shule ya msingi.

[email protected]