Habari MsetoSiasa

Prof Kibwana atakiwa kuomba msamaha kwa kumkejeli Kalonzo

January 8th, 2019 1 min read

Na STEPHEN MUTHINI

GAVANA wa Kaunti ya Makueni, Prof Kivutha Kibwana, ameambiwa aombe msamaha kwa kumkosoa Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka.

Akizungumza Machakos, katibu mwandalizi wa chama hicho, tawi la Makueni, Bw Jackson Ngovi alisema inasikitisha kwamba gavana huyo alichaguliwa kwa tikiti ya Wiper ilhali anamharibia sifa hadharani kiongozi wa chama.

“Kwa hivyo tunamwomba gavana huyo aamue kuhusu msimamo wake wa kisiasa na aachane na Wiper kwani hatutamruhusu kutuvurugia chama akiwa ndani,” akasema Bw Ngovi.

Katibu huyo alisema matamshi ya Prof Kibwana dhidi ya Bw Musyoka hayaharibu tu sifa ya makamu huyo wa rais wa zamani bali pia ni kejeli kwa jamii nzima ya Wakamba.

Alikosoa jinsi Prof Kubwana alivyoingiza jina la aliyekuwa kigogo wa siasa za Ukambani, marehemu Mulu Mutisya, kwenye matamshi yake dhidi ya Bw Musyoka.

Hivi majuzi Prof Kibwana alinukuliwa kwenye vyombo vya habari akimkashifu Bw Musyoka kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa uongozi wa jamii ya Wakamba alioachiwa na marehemu Mutisya. Bw Ngovi alisema jamii hiyo inamfuata Bw Musyoka kikamilifu na hakuna kitakachobadili msimamo huo.

na kuonya yeyote aliye na nia ya kuvuruga azimio la Bw Musyoka la urais 2022 kwamba watapingwa vilivyo.

Alimtaka gavana huyo atangaze msimamo wake wa kisiasa bila kuvuruga Wiper na kutoa wito kwa Bw Musyoka atafute uungwaji mkono kutoka maeneo mengine kitaifa huku wandani wake wakimpigia debe katika eneo la Ukambani.