HabariSiasa

Prof Kibwana tosha 2022, Wakenya mitandaoni waamua

September 4th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

WAKENYA sasa wanataka Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana alazimishwe kuwa Rais akikosa kuwania, baada ya kufurahishwa na uongozi wa uadilifu na hekima ya kufanya maendeleo katika kaunti yake.

Wiki chache baada ya kupokea sifa tele alipoandaa kongamano la mafunzo kuhusu mbinu za uongozi bora kwa magavana wengine, Prof Kibwana sasa amerejea vinywani mwa Wakenya kwa hali nzuri, na sasa wanataka awe kiongozi wa nchi ili kusuluhisha matatizo mengi ambayo taifa linakumbana nayo.

Kampeni hii mpya ya kumtaka Gavana Kibwana kuongoza Kenya kama Rais aidha kwa hiari yake ama kwa kulazimishwa zilianza Jumanne, baada ya kiongozi huyo kuchapisha picha kwenye ukurasa wake wa Facebook akiwa na watoto.

Katika picha hiyo, Prof Kibwana amepiga magoti na kuinama pamoja na watoto wanaosoma kitabu, huku akikaa kama anayewaelekeza kusoma, nao walimu wakitazama kwa tabasamu.

Gavana Prof Kivutha Kibwana atangamana na baadhi ya wanafunzi wa chekechea alipozindua mradi wa vitabu katika wadi ya Tulimani, Kaunti ya Makueni Septemba 4, 2018. Picha/ Hisani

Wakenya hawakuweza kuficha furaha yao walipoona profesa mzima akipiga magoti kwenye nyasi licha ya hadhi yake, wengi wakiishia kulaumu magavana wao wakimlinganisha na Prof Kibwana.

“Nadhani Kenya sasa inafaa kumfanya mwanamume huyu Rais. Ni muungwana sana wa kujishusha na aliye karibu na mwananchi,” akasema Kimondo Musyoki.

Lakini Masita Atinda hakupita njia ndefu kupitisha ujumbe wake “huyu gavana anafaa kulazimishwa kuwa Rais hata akikataa,” akasema.

Wengine walitaka kiongozi huyo atuzwe hata zaidi, wakiona kuwa urais pekee hautatosha kumlipa kwa hekima na busara yake.

“Gavana Kivutha anafaa kupewa tuzo ya Nobel kwa upole na huduma njema kwa binadamu, hata anafaa kuwekwa katika kitabu cha rekodi cha Guinnes kwa kuwa matendo yake mazuri yamezidi,” akasema Alex Nzioki.

Mmoja wa wanafunzi wa chekechea ainua kitabu baada ya Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana kuzindua mradi wa vitabu kwa watoto wote wa kaunti hiyo. Picha/ Hisani

“Kivutha Kibwana uongozi wako unafaa kuwa wa taifa zima, namaanisha RAIS WA JAMHURI YA KENYA, tafadhali gombea mnamo 2022. Mimi na mamilioni ya Wakenya wengine pamoja na kijiji chetu tutakuunga mkono asilimia 100,” akasema Watson Junior.

“Mwanamume huyu ana busara ya magavana wote 47 pamoja na mawaziri katika akili zake, ametumwa na Mungu na ambariki,” akasema Bee Masters Peace.

Kwa wengine, picha ya gavana huyo iliibua kumbukumbu za awali wakati alionekana akimbeba mtoto.

“Nadhani Kenya inafaa kuongozwa na mtu wa upole wa kiasi hiki, kuna wakati nilimwona akimbeba mtoto mgongoni. Naomba tu uwanie urais,” Jomo Amoh hakuficha.

Jefrito Ibn Jeefar alisema “kazi nzuri, wewe ndiye aina ya kiongozi wanayetaka Wakenya, tafadhali gombea kiti cha Urais ifikapo 2022, hakuna mwingine mwenye uwezo wa kubishana nawe.”